Macron awakaribisha viongozi wa Ulaya kuizungumzia Ukraine
27 Machi 2025Washirika hao wa Ukraine kutoka kote barani Ulaya wamekusanyika kwa mazungumzo mjini Paris kuhusu jinsi ya kuimarisha uungaji mkono kwa Ukraine wakati nchi hiyo ikishinikiza kusitishwa kwa mapigano na Urusi, na wakati huohuo mkutano huo unazingatia mapendekezo ya kupeleka wanajeshi wa Ulaya nchini Ukraine sanjari na makubaliano yoyote ya amani. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amependekeza kwamba kikosi hicho cha jeshi kinaweza kupelekwa katika miji mahali kwengine muhimu.
Miongoni mwa wakuu wa nchi za Ulaya wanaohudhuria mkutano huo ni Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky, Kansela wa Ujerumani anayemaliza muda wake Olaf Scholz, Mawaziri Wakuu wa Uingereza Keir Starmer, wa Poland Donald Tusk, Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen na wa Italia Giorgia Meloni pamoja na katibu mkuu wa jumuiya ya NATO na makamu wa rais wa Uturuki Cevdet Yılmaz.
Soma pia: Ukraine kupokea ahadi mpya za misaada Paris
Mkutano huo unafanyika katika wakati muhimu wa vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu, kati ya Urusi na Ukraine huku juhudi za kidiplomasia zikiimarishwa za kusitisha mapigano, kutokana na shinikizo kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump.
Huu ni mkutano wa tatu wa aina hiyo uliopewa jina na Ufaransa na Uingereza kuwa ni mkutano wa "Muungano wa walio tayari", unaoangazia wasiwasi uliopo miongoni mwa nchi za Ulaya kwamba Marekani haiiwakilishi tena ngome imara ya kuipa msaada Ukraine katika mapambano yake dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Soma pia: Ukraine na Urusi zaendelea kutupiana lawama
Ofisi ya Rais wa Ufaransa imesema ingawa Marekani haishiriki kwenye mkutano huo lakini matokeo ya mkutano huo yatawasilishwa kwa utawala wa Marekani na kwamba rais Macron alizungumza na Rais wa Marekani Donald Trump kabla ya kuanza mkutano huo.
Mkutano huo unafanyika baada ya rais wa Ukraine Volodymir Zelenskiy kukubali mapema mwezi huu kuendelea na mazungumzo ya kusitisha mapigano ili kuhakikishiwa kuwa nchi yake inapata tena usaidizi wa Marekani na pia ugavi wa taarifa za kijasusi kutoka kwenye taifa hilo kubwa.
Vyanzo: RTRE/AFP
Mhariri: Jacob Safari