Macron awaambia wenzake wa EU alichozungumza na Trump
26 Februari 2025Kwenye mkutano huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwahimiza wenzake wa Ulaya, ambao nchi zao zimeachwa nje kwenye mazungumzo ya hivi karibuni kuhusu Ukraine kati ya wawakilishi wa Marekani na Urusi kwa kuwaambia kuwa wanatakiwa kusisitiza juu ya bara Ulaya kushirikishwa kwa karibu katika mazungumzo yanayohusu vita vya Ukraine.
Soma pia: Rais Donald Trump awataka Putin na Zelensky kukutana
Rais wa Baraza la Ulaya António Costa, ndiye aliyeandaa mkutano huo amesema ulikuwa wa manufaa kwa ajili ya maandalizi ya mkutano maalum wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika wiki ijayo kujadili jinsi ya kukabiliana na mabadiliko katika sera ya Marekani kuhusu vita katika Ukraine.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kwenye mazungumzo yake na Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumatatu pia alizungumzia juu ya kuiunga mkono dhana ya kupelekwa wanajeshi wa Ulaya nchini Ukraine kwa ajili ya kulinda amani.
Soma pia: Urusi na Ukraine zashambuliana vikali
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, ambaye anatarajiwa kufanya mazungumzo na Trump kesho Alhamisi, amesema nchi yake iko tayari kuwapeleka wanajeshi wake nchini Ukraine kama sehemu ya ujumbe wa kulinda amani baada ya vita.
Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema nchi yake haiwezi kulikubali pendekezo lolote linalohusu kupelekwa nchini Ukraine wanajeshi wa Ulaya amesema, wazo kama hilol inalenga tu kuuchochea mgogoro na kutengeneza hali ngumu ya kuutatua mgogoro huo.
Marais Macron na Trump walionyesha tofauti kubwa kwenye mitazamo yao siku ya Jumatatu kuhusiana na swala la Ukraine, hali inayofichua kuwepo mgawanyiko kati ya Marekani na bara Ulaya baada ya Rais wa Marekani kutangaza kwamba anayo njia ya haraka pamoja na Urusi ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano haraka.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk, amesema viongozi wa Ulaya wanapaswa kupinga "kujisalimisha" kwa Urusi kuhusiana na swala la Ukraine baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuamua kushirikiana na Urusi.
Soma pia: Russia, USA, zakubaliana kufikisha mwisho vita Ukraine
Wakati hayo yanaendelea Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Jumatano anatumai kuzuru mjini Washington siku ya Ijumaa. Amesema ziara hiyo ni kwa ajili ya kufikia makubaliano ya madini na Marekani na pia kujadiliana kuhusu msaada wa siku zijazo kwa Ukraine na Rais Donald Trump.
Trump ameitaka Ukraine kutoa ruhusa kwa Marekani kuyatia mikononi madini yake adimu ili kufidia mabilioni ya dola ya msaada iliyopokea wakati wa vita chini ya utawala wa Rais aliyeondoka Joe Biden.
Vyanzo: AFP/DPA/RTRE