Macron apendekeza mkutano wa Putin, Zelensky ufanyike Geneva
19 Agosti 2025Akizungumza Jumanne na kituo cha habari cha Ufaransa, LCI, Macron ametangaza kuwa mkutano wa kilele kati ya viongozi wa Urusi na Ukraine utafanyika Ulaya.
Macron ameyasema hayo baada ya Rais wa Marekani Donald Trump, kufanya mazungumzo na viongozi wa Ulaya, Jumuiya ya Kujihami ya NATO na Zelensky mjini Washington Jumatatu.
''Pengine mkutano utafanyika Uswisi. Ningependekeza Geneva au nchi nyingine. Kesho kuna mkutano. Tutaanza kuangalia suala la hakikisho la usalama. Kazi hii kwa kiasi fulani ni sharti kwa mikutano yote,'' alifafanua Macron.
Baada ya kukutana na viongozi hao, Trump alimpigia simu Putin kujadiliana kuhusu mazungumzo ya ana kwa ana kati ya viongozi wa Urusi na Ukraine.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, amesema mkutano huo unaweza kufanyika ndani ya wiki mbili zijazo.