Macron: Natumai Trump atachukua hatua kali dhidi ya Putin
26 Mei 2025Mashambulizi hayo yaliyotokea pia katika maeneo mengine ya Ukraine, yanafanyika licha ya hatua zinazochukuliwa na Marekani za kuyashinikiza mataifa yote mawili hasimu kufikia makubaliano ya kusitisha vita.
Macron aliwaambia waandishi habari mjini Hanoi, kituo cha mwanzo cha ziara yake Kusini Mashariki mwa bara Asia, kwamba anaamini sasa Trump anatambua, muda wote Putin amekuwa akimdanganya. Macron amependekeza Urusi iwekewe vikwazo zaidi kuishinikiza iachane na mashambulizi yake Ukraine.
Awali Trump alimkosoa mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kwa kumuita mwendawazimu baada ya taifa hilo kuishambulia Ukraine kwa makombora na droni na kusababisha vifo vya watu 13.
Mwezi Mei mwaka huu rais Emmanuel Macron alisafiri Kyiv na viongozi wengine wa Ulaya kuipa Urusi muda wa mwisho ulioridhiwa na Marekani kuishinikiza kukubali mpango wa usitishwaji mapigano.