Macron aenda Marekani kwa ajili ya mazungumzo na Trump
24 Februari 2025Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anakutana hii leo na Rais Donald Trump wa Marekani mjini Washington, akisema atampatia "pendekezo la hatua za kuchukua dhidi ya kitisho cha Urusi barani Ulaya na kuhakikisha amani nchini Ukraine".
Macron analenga kumshawsihi Trump wakati watakapokutana kuwajumuisha viongozi wa Ulaya kwenye mazungumzo kati ya Urusi na Marekani wakati ambapo leo imetimia miaka tatu tangu kuanza vita vya Ukraine.
Mshauri wa Rais Macron amesema kiongozi huyo aidha ataishawishi Marekani kuendelea kuiunga mkono Ukraine, kuheshimu uhuru wake na kuhakikisha kwamba maslahi ya Ulaya yanazingatiwa.
Trump aliibua mshituko kote barani Ulaya baada ya kutangaza nia ya kurejesha juhudi za kidiplomasia na Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kuzungumza naye bila ya kuihusisha Ulaya ama Kyiv.