Machozi, shangwe Wapalestina walioachiwa Ukingo wa Magharibi
1 Februari 2025Akishuka kwenye basi pamoja na wafungwa wengine wa Kipalestina 25 walioachiliwa huru siku ya Jumamosi baada ya kutumikia kifungo cha miaka 23 nchini Israel, Ata Abdelghani alikuwa na zaidi ya uhuru wake mbele yake.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 55 aliweza pia kuwakumbatia watoto wake mapacha, Zain na Zaid, kwa mara ya kwanza.
Hilo liliwezeshwa na hatua ya kuachiliwa kwake katika mabadilishano ya wafungwa na mateka kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya Januari katika Ukanda wa Gaza yaliyokubaliwa na Israel na Hamas.
Mapacha hao, sasa wakiwa na miaka 10, walizaliwa wakati Abdelghani akiwa gerezani baada ya mbegu zake kusafirishwa kutoka gerezani kwake.
Alikuwa anatumikia kifungo cha maisha kutokana na mashtaka kadhaa, ikiwa ni pamoja na mauaji na uanachama wa shirika haramu, kulingana na orodha iliyotolewa na wizara ya haki za Israel.
"Watoto hawa ni mabalozi wa uhuru, kizazi kijacho," alisema Abdelghani alipowakumbatia watoto kwa nguvu.
Katika awamu hiyo ya kuachiliwa wafungwa siku ya Jumamosi, tangu kuanza kwa makubaliano ya kusitisha mapigano ya Gaza mnamo Januari 19, umati mkubwa ulikusanyika kuwaona wafungwa 25 wa Kipalestina walioachiliwa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel.
Soma pia: Hamas na Israel kubadilishana tena mateka na wafungwa Jumamosi
Wakiwa wamevaa sare za gerezani za rangi ya kijivu na vichwa vyao vikiwa vimenyolewa, wafungwa hao walionekana kuchoka walipofika, lakini wengi waliinuliwa juu ya mabega ya watu na kubebwa kwa shangwe kama mashujaa.
"Ni vigumu kuelezea kwa maneno," alisema Abdelghani. "Mawazo yangu yamezagaa. Nahitaji utulivu mkubwa kujidhibiti, kudhibiti hisia zangu, kumeza wakati huu mkubwa."
Aliongeza kusema kwamba hali gerezani ilikuwa "ngumu, ya kusikitisha." Jumla ya wafungwa 183, karibu wote wakiwa ni Wapalestina na Mmisri mmoja, waliachiwa huru siku ya Jumamosi.
Soma pia: Mateka 4 wa Israel na wafungwa 200 wa Kipalestina waachiwa
Saba waliokuwa wanatumikia kifungo cha maisha na Mmisri walifukuzwa kwenda Misri, kulingana na Chama cha Wafungwa wa Kipalestina. Kati ya wengine, 150 walipelekwa Gaza.
Wafungwa hao walifunguliwa kwa kubadilishana na mateka watatu wa Kiyahudi waliotekwa nyara wakati wa shambulio lisilo la kawaida la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023.
Akutana na watoto wake baada ya miaka 22
Riad Marshoud, mwingine aliyeachiwa, alilia wakati akiwakumbatia watoto wake wawili, ambao walikuwa wadogo sana wakati alipokamatwa miaka 22 iliyopita.
Baada ya kuwaumbatia kwa nguvu, aliketi kwenye kiti huku jamaa zake wakifanya mazungumzo ya video na jamaa na wakwe ambao hawakuweza kufika kumuona akiachiliwa.
Jamaa mmoja alikuwa Jordan na mwingine Umoja wa Falme za Kiarabu.
Wote walijaribu kumwona Marshoud aliyekuwa ameduwaa na kuchoka lakini alifurahi sana alipopokea pongezi.
"Wakati wa kwanza milango ya basi ilipofunguliwa na mimi kutoka nje ulikuwa ngumu sana -- ni ngumu kuielezea kwa maneno tu," aliuambia umati.
Soma pia: Ripoti ya UN yasema Israel inawatesa wafungwa wa Kipalestina
Umati mkubwa uliojitokeza kumwona Marshoud ulijitenga wakati baba yake alipofika akiwa na keffiyeh ya kitamaduni kichwani. Baba alimpokea mwanawe kwa mabusu ya machozi.
Marshoud alikamatwa kwa mashtaka ya kuwa mwanachama wa shirika haramu, kumiliki risasi na njama ya kutenda mauaji, kulingana na wizara ya sheria ya Israel.
Baada ya familia mjini Ramallah kuwapeleka jamaa zao walioachiwa huru nyumbani, basi tatu za wafungwa zilifika katika mji wa Khan Yunis, kusini mwa Gaza, aliripoti mwandishi wa AFP.
Wafungwa 150 walipokelewa kwa vifijo na nderemo kutoka kwa umati baada ya kushuka kutoka kwenye mabasi - "Kwa damu na roho, tutakukomboa, mfungwa!"
Chanzo: AFP