Machafuko yazuka tena Mashariki mwa Kongo
26 Machi 2025Mapigano mapya yamezuka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo huku mataifa jirani yakijaribu kuufufua mchakato wa kutafuta amani. Waasi wa kundi la M23 wamefutilia mbali ahadi ya kujiondoa katika maeneo wanayoyadhibiti na kulituhumu jeshi la Kongo kwa kufanya uchokozi. Wakati hayo yakiarifiwa watu wawili wameuawa katika mazishi ya mwanamuziki maarufu wa Kongo.
Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamepambana na waasi wanaoegemea upande wa serikali jana Jumanne huku nchi za kikanda zikijaribu kuupa msukumo mpya mchakato wa kutafuta amani ambao umekuwa ukisuasua. Waasi wa M23 wamefanikiwa kuiteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Kongo tangu Januari, huku maalfu ya vifo vikiripotiwa na mamia kwa maalfu ya watu wakilazimika kuyakimbia makazi yao.
Viongozi wa nchi za ukanda wa kusini na mashariki mwa Afrika mara kwa mara wamekuwa wakifanya juhudi za kidiplomasia kuutanzua mgogoro wa Kongo huku kukiwa na hofu huenda ukasambaa na kuwa vita vikubwa vya kikanda.
Pigo la hivi karibuni kwa juhudi hizo lilitokea Jumatatu wiki hii wakati waasi wa M23 walipofutilia mbali ahadi yao ya kuondoka kutoka mji wa kimkakati wa Walikale na kulituhumu jeshi la Kongo kwa kushindwa kusitisha operesheni yake katika mji huo. Kwa mujibu wa wakaazi, waasi hao walipambana jana Jumanne na wapiganaji waasi wanaofahamika kama Wazalendo katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Muhindo Tafuteni, mwanaharakati wa shirika la kijamii amesema huko Kivu Kaskazini, siku ya pili ya makabiliano yalishuhudiwa karibu na fukwe za Ziwa Edward, linalopatikana katika mpaka kati ya Kongo na Uganda. Katika mkoa wa Kivu Kusini wakazi wamesema mapigano yalitokea katika miji kadhaa kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo hilo, Bukavu, ambao waasi wa M23 waliuteka mwezi Januari.
Watu wawili wauliwa mashariki mwa Kongo
Wakati hayo yakiarifiwa polisi mashariki mwa Kongo wamewaua watu wawili jana Jumanne wakati walipowafyetulia risasi waombolezaji waliokuwa katika mazishi ya mwanamuziki aliyeuwawa aliyefahamika kwa kuikosoa serikali na waasi wa M23. Hayo ni kwa mujibu wa watu walioshuhudia.
Maalfu ya raia wa Kongo walikuwa wamekusanyika kutoa heshima zao za mwisho kwa Delcat Idengo, wakilifuata jeneza lake lililokuwa na muundo wa gari kupitia barabara za mji alikozaliwa wa Beni.
Mchana kutwa waombolezaji walipiga kelele wakiwalaani waasi wa M23 ambao wanawatuhumu kwa kumuua Idengo mwezi uliopita baada ya kuudhibiti mji wa Goma, na kwa upande mwingine wakiituhumu serikali kwa kumkamata mara kadhaa. M23 haijatoa kauli moja kwa moja kujibu madai hayo kwamba wapiganaji wake walimuua Idengo.
Soma pia: M23 waendelea kuudhibiti mji wa Walikale
Machafuko yalizuka katika mji wa Beni, unaopatikana karibu kilometa 200 kaskazini mwa mji wa Goma na ulio chini ya udhibiti wa serikali, baada ya polisi kufyetua risasi dhidi ya umati wa watu waliojawa na ghadhabu. Mashuhuda wanasema waliona watu wawili wameuliwa. Jean-Pierre Kasma ni mmoja wa waombolezaji waliokuwa katika eneo la mazishi.
Jean-Pierre Kasma ni mmoja wa waombolezaji waliokuwa katika eneo la mazishi. "Kwa wakati huu, nahisi ghadhabu. Nimekasirika sana. Nimevunjika moyo sana kwa sababu ndugu, rafiki, mtu anayejiita raia wa Kongo bwana Corneille Nangaa, anakuja, inasemakana kwa nia ya kutukomboa, lakini tumeshtuka kumuona akiwasili na kuanza kutuua. Nahisi hasira. Nahisi nimevunjwa moyo na yeye kwa sababu kwa mtu ambaye ni raia wa Kongo, inasikitisha na jambo la kujutia kwamba anaweza kuwaua watu mwenyewe."
Meya wa mji wa Beni, Jacob Nyofondo Tekodale, amewaambia waandishi habari kwamba Idengo alikuwa amezikwa huku maalfu ya watu wakishuhudia na kujuta kwamba matukio kadhaa yalijitokeza wakati wa mazishi yake.
Idengo, ambaye jina lake halisi ni Delphin Katembo, alikuwa na mashabiki wengi waliompenda sana kwa nyimbo zake zilizoikosoa serikali. Alitiwa nguvuni mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na mwaka 2021 kwa kumtusi Rais Felix Tshisekedi, na akatiwa mbaroni tena mwaka jana wakati wa maandamano. Alitoroka gereza kuu la mji wa Goma pamoja na maalfu ya wafungwa wengine wakati M23 walipouteka mji huo mwezi Januari.