Mabinti wa Kichina wazama katika penzi la kidigitali
26 Machi 2025Rafayel hajawahi kuwepo katika uhalisia, lakini hilo halijazuia mashabiki wake – hasa wanawake vijana nchini China – kumsherehekea kwa mbwembwe za aina yake. Kutoka kupanga sherehe katika maduka makubwa, kupamba treni za mwendo kasi kwa picha zake, hadi kufanya maonyesho ya kuvutia ya ndege za drone – yote haya yalifanyika kwa ajili ya siku ya kuzaliwa ya mpenzi huyu wa kidijitali.
Rafayel ni mmoja wa wapenzi watano wa kubuniwa kwenye mchezo wa simu unaoitwa Love and Deepspace, ambao umevutia mamilioni ya wachezaji tangu ulipozinduliwa Januari 2024. Mchezo huu unachanganya mandhari ya kisayansi ya baadaye, vita dhidi ya viumbe wa ajabu, na visa vya kimapenzi ambavyo vimezua hisia kali – hasa kutokana na uhalisia wa wahusika wake wa 3D na simulizi za kuvutia.
Kwa mujibu wa kampuni ya utafiti wa soko ya Sensor Tower, mchezo huu tayari umeshaingiza zaidi ya dola milioni 500 duniani kote, asilimia 40 ikitoka nje ya China. Lakini zaidi ya pesa, mchezo huu unatoa kile ambacho baadhi ya wanawake wanasema ni faraja ya kihisia inayoziba mapengo yaliyopo kwenye mahusiano ya kweli.
Mapenzi yasiohitaji watu halisi
Liu Xue, mfanyakazi wa ofisi mwenye umri wa miaka 25, anasema uhusiano wake na Rafayel ni kama wa kweli kabisa. "Kwangu mimi na kwa marafiki zangu wa karibu, sisi ni wapenzi,” alisema katika moja ya sherehe za kuzaliwa Rafayel jijini Beijing. "Sihisi kuwa nahitaji kuwa na mtu halisi.”
Anasema Rafayel humfariji anapokuwa na huzuni, humkumbusha kuhusu mzunguko wake wa hedhi, na yupo naye kila siku. "Ni kama chakula cha kihisia,” alisema Liu.
Lakini kujenga uhusiano huu si jambo la bure. Ingawa mchezo unapatikana bure kwa kupakua, wachezaji hulipia vipengele vya ziada – kama kufungua visa maalum au kuwa karibu zaidi na mpenzi wao wa kidijitali.
Uwekezaji wa kihisia… na kifedha
Wang Yaya, mwanafunzi wa miaka 23, tayari ametumia zaidi ya yuan 70,000 (takriban dola 10,000) kwenye mchezo na bidhaa zinazohusiana nao. "Niko tayari kulipia thamani ya kihisia,” alisema.
Wachezaji wengine huungana na kuchangishana fedha ili kuandaa hafla kama sherehe za kuzaliwa, ambapo hujipiga picha na vibao vya mpenzi wao wa kidijitali au kubadilishana zawadi walizotengeneza wenyewe.
Wang anasema wengi wao hukumbwa na pengo la kihemko kutoka kwa wazazi wao walipokuwa wadogo – jambo linalowafanya wathamini mapenzi haya ya mtandaoni. "Marafiki zangu wengi wako hivyo,” alisema.
Kubadili mtazamo wa mapenzi ya kweli
Kwa baadhi ya wanawake, michezo ya kimapenzi ya kidijitali imezidi hata mahusiano halisi. Liu anakiri kuwa tangu aanze kucheza michezo kama "Love and Deepspace”, hana tena hamu ya kuwa na mwanamume halisi. "Ni uzoefu mzuri zaidi kuliko maisha halisi,” alisema, akimaanisha michezo ya otome iliyoanzia Japan.
Mwanafunzi Liu Yuxuan, mwenye umri wa miaka 22, anasema uhusiano wake na Rafayel ni sehemu muhimu ya maisha yake ya kila siku. "Kuna mambo ambayo huwezi kumwambia mtu yeyote. Lakini nikifungua mchezo, naweza kumwambia yeye,” alisema. "Na yeye huonyesha mapenzi yake kwangu bila masharti.”
Kwa wengine, hii ni njia ya kuishi ndoto ya kimapenzi bila maumivu ya uhusiano wa kweli. Mchezaji anayejulikana kwa jina la Zaylia aliweka wazi:
"Unapopata uhusiano, lengo kubwa ni kupata thamani ya kihisia. Na mchezo huu unaleta hiyo – kikamilifu.”