Bayern Munich kuanza mbio za ubingwa dhidi ya Leipzig
21 Agosti 2025Ingawa miamba hao wa Ujerumani walikuwa na muda mfupi wa maandalizi kutokana na kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la Vilabu nchini Marekani, bado wanabeba matumaini makubwa ya kuanza msimu kwa ushindi, hasa kutokana na rekodi yao nzuri katika mechi za ufunguzi.
Wakiwa wameshinda taji la ligi mara 12 katika kipindi cha miaka 13 iliyopita, "The Bavarians" wameshinda taji hilo mara nyingi zaidi ya klabu nyingine yoyote, huku wakiongezwa nguvu na ujio wa Luis Diaz kutoka Liverpool kwa kitita cha yuro milioni 70, pamoja na wachezaji wengine wa kimataifa wa Ujerumani Jonathan Tah na Tom Bischof.
BvB na Bayern bado wachovu baada ya Kombe la Dunia la Vilabu
Baada ya kushiriki kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Vilabu iliofanyika nchini Marekani kuanzia 15 Juni hadi 13 Julai 2025, Bayern Munich pamoja na Borussia Dortmund walipata muda mfupi sana wa maandalizi kabla ya msimu mpya wa Bundesliga kuanza.
Bayern walipata kombe lao la kwanza msimu huu wiki iliyopita la Supercup, baada ya kuwashinda mabingwa wa Kombe la Ujerumani VfB Stuttgart 2-1 katika mechi iliyochezwa siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa MHP Arena, licha ya baadhi ya wachezaji kuwa na maumivu ya misuli.
Kwa upande mwengine, Bayer Leverkusen iko kwenye mageuzi makubwa baada ya kuondoka kwa kocha Xabi Alonso, aliyewaongoza kuchukua ubingwa wa Bundesliga mwaka 2024 bila ya kufungwa, lakini pia mchezaji nyota Florian Wirtz, aliyekwenda Liverpool na wachezaji wengine muhimu.
Viatu vya Alonso, vitamtosha ten Hag?
Kocha mpya Erick Ten Haag anayemrithi Alonso ana kibarua kigumu cha kukiongoza kikosi hicho ambacho pia kimeondokewa na kiungo muhimu Granit Xhaka, na uwezekano unatajwa kuwa mdogo wa kuleta ushindani katika mbio za ubingwa msimu huu. Wanaanza kampeni yao ya ligi Jumamosi hii dhidi ya wageni wa Hoffenheim.
Wapinzani wa Bayern Munich, Borussia Dortmund, wataanza msimu mpya wa Bundesliga kwa mechi ya ugenini dhidi ya St. Pauli siku ya Jumamosi, tarehe 23 Agosti 2025 kwenye uwanja wa Millerntor-Stadion, Hamburg.
Kocha Niko Kovac, aliyechukua usukani katikati mwa msimu uliopita, aliliimarisha jahazi na kuwaongoza kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Tangu wakati huo amewaleta wachezaji Jobe Bellingham kiungo kutoka Sunderland na kakake mdogo wa Jude Bellingham, na beki wa kulia kutoka Manchester City Yan Couto, akilenga kujiimarisha zaidi.