Maaskofu wa Kongo wasema amani ni muhimu Kivu Kaskazini
13 Februari 2025Wajumbe hao wa makanisa waliongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki katika jimbo la Kivu Kaskazini, Askofu Ngumbi Ngengele walitilia mkazo haja ya kushirikiana ili kuhakikisha amani inarejea Goma na maeneo mengine yanayoathiriwa na machafuko hayo.
Askofu Donatien Nshole, katibu Mkuu wa Kongamano la Maaskofu wa Kongo,CENCO , amesema kuna mambo mengi ya kujadili kuhusu mzozo huu iwapo pande husika zitageukia meza ya mazungumzo kwa kutafuta amani.
"Tulielewa kuwa kuna mambo mengi ambayo yanaweza kutatuliwa ikiwa Wakongo wataketi katika meza moja ya mazungumzo ili kuutatua mzozo huu. Pia kwetu mazungumzo hayo yalilenga kuwaonesha hofu ya Wakongomani kuhusu kuligawana taifa hili la Kongo. Kuhusu uporaji haramu wa maliasili huko pia tulikuwa na majibu ya uhakika na kwamba hawana lengo la kuigawana DRC vipande vipande", alisema Nshole.
"Usitishwaji haraka wa vita"
Kwa zaidi ya saa tatu wajumbe hao wa Kanisa Katoliki na Wakristo wa madhehebu mbalimbali hapa nchini walijadili njia za amani katika mzozo huo unaosambaa mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Kulingana na Askofu Donatien N'SHOLE, baada ya kikao hicho na viongozi wa M23, wajumbe hao walionyesha mataumaini kuhusu usitishwaji wa mapigano na kuanzishwa kwa safari za ndege kwenye uwanja ndege wa Goma, jambo ambalo linaweza kusaidia kurejesha hali ya kawaida na kuimarisha uchumi wa wakazi.
"Pia fursa hii ni kwa ajili ya kutetea kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege wa Goma na bandari, lakini pia usitishwaji wa vita haraka iwezekanavyo kwa sababu bado tunaamini kwamba suluhu ya mgogoro huu sio ya kijeshi."
Mapigano yaendelea kupamba moto Kivu Kusini
Ikiwa bado hali ya usalama inaaendelea kuwa tete katika baadhi ya maeneo mjini Goma, viongozi hao wa kidini walijadiliana kuhusu mikakati ya kuumaliza mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini kati ya serikali ya Kongo na M23 ambao bado wanaendelea na mapigano katika jimbo jirani la Kivu Kusini.
Wakati huo huo, Guel Mamlaka afisa mwandamizi na mjumbe wa shirika jipya la kiraia nchini Kongo, amesema usalama wa wananchi ndio kipaumbele katika hali hii inayoshuhudiwa kuwa mbaya zaidi.
"Viongozi hao wa Kanisa Katoliki na Kiprotestanti, ikiwa wanadhani kuwa na uwezo wa kutatua mzozo huu, hakuna shida! Sisi kama raia tunaomba amani na usalama pekee, lakini iwapo kikao hicho ni kwa ajili ya kutumia tu bure pesa za umma hakutakuwa na matunda bora. Muhimu kwetu ni amani iweze kurudi."
Hali mbaya ya kibinadamu
Licha ya juhudi zote zinazofanywa na viongozi wapya kurejesha utulivu katika mji wa Goma, maelfu ya raia bado wanaendelea kuhangaika kufuatia ongezeko la visa vya uhalifu vinavyofanywa na makundi ya watu wenye silaha wanaozishambulia nyumba za raia hao kwa risasi.
Aidha, fuduma za benki na shule bado hazijaanza kutolewa mjini Goma, licha ya wito wa uongozi wa muungano wa waasi wa AFC/M23 kuwataka wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni mwanzoni mwa wiki hii.