Maandamano ya kupinga ugaidi.
22 Novemba 2004Waislamu hapa nchini Ujerumani aghalabu wanaishi katika jamii zao,wanazungumza ,lugha zao,wana misikiti yao,hospitali, na hata baadhi ya majina ya mitaa katika seheme wanapoishi yanaandikwa katika lugha mbili, kwa jumla waislamu hapa nchini wana utamaduni wao. Serikali ya Ujerumani inawaunga mkono kwa kupitisha sheria juu ya kuendelezza utamaduni huo
Baadhi ya vyombo vya habari vimechapisha makala juu ya kile kinachoitwa wageni wa kutisha na wa ajabu yaani waislamu. Makala hizo siyo za busara hasa wakati huu.
Hapa nchini pana waislamu wapatao milioni 3 na laki mbili.Idadi kubwa miongoni mwao ni waturuki. Baadhi yao sasa wanatuhumiwa kuwa watumishi wa Osama Bin Laden.
Msimamo huo unatokana na matukio ya nchi jirani ya Uholanzi ambapo mtunga filamu Theo Van Gogh aliuawa na mwislamu mwenye itikadi kali hivi karibuni. Tukio hilo hapa nchini Ujerumani linatumiwa na watu wanaodai kwamba kuwepo kwa idadi ,kubwa ya waislamu ni jambo la hatari. Sasa maswali mengi yanaulizwa juu ya jamii ya waislamu wa hapa nchini; maswali juu ya lugha inayotumiwa wakati wa kufunga sala, juu ya wanawake wa nk. Maswali kama hayo yanahatarisha moyo wa kuzileta pamoja tamaduni mbalimbali katika jamii.
Sasa wanasiasa wa vyama vyote vya hapa nchini wanatoa miito na maoni juu ya waislamu kana kwamba kuwepo kwa waislamu hapa nchini ni jambo jipya. Mambo yanayozungumziwa katika vyombo vya habari juu ya dini ya kiislamu siyo mapya asilani hapa nchini. Ni mambo yanayofahamika kwa muda mrefu, hayakungumziwa sana hadhari kutokana na sababu za utepetevu na maono finyu.
Ipo hali ya kutoelewanaa baina ya wajerumani na jamii ya waislamu. Mwislamu ambaye hajui kijerumani hataweza kufanya hivyo katika kipindi cha wiki mbili ama tatu.Na mwislamu ambaye hajajumuika na wajerumani hatafanikiwa kufanya hivyo mnamo mwezi mmoja ama miwili. Hayo ni mambo yasiyoeleweka vizuri miongoni mwa baadhi ya wajerumani ikiwa pamoja na vyombo vya habari. Walio wengi hapa nchini yaani wajerumani wanawaweka waislamu wote katika kundi moja.
Watu hao wanadai kwamba waislamu wanajenga jamii nyingine sambamba na ya wajerumani. Mtazamo huo hautasaidia katika kujenga mawasiliano baina ya tamaduni mbalimbali hapa nchini.
Maandamano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki yalikuwa na lengo la kuonyesha kwamba ipo tofauti baina ya waislamu wa dhati na wale wanaofuata siasa kali na kufanya matendo ya kigaidi. Waislamu wa hapa nchini kwenye maandamano yao walilaani ugaidi wa kila aina. Wamesema anayefuata dini ya kiislamu kwa dhati hahusiani hata kidogo na Osama Bin Laden.