Maandamano ya kimataifa dhidi ya vita vya Iraq:
21 Machi 2004Matangazo
NEW YORK: Hapo jana ukitimiza mwaka mmoja tangu vianze vita vya Iraq watu kwa maelfu kote duniani wamefanya maandamano makubwa ya kupinga vita na kutoa mwito wa amani. Peke yake mjini New York waliandamana watu zaidi ya 100,000 wakiitaka Marekani ihamishe wanajeshi wake kutoka Iraq. Maandamano makubwa mengine yalifanyika Uingereza, Poland, Uspania, Uitalia na Australia, zikiwa ni nchi ambazo serikali zake zimepeleka wanajeshi wao Iraq. Maandamano yalifanyika pia katika miji kadha mikubwa barani Asia na Arabuni. Katika maandamano makubwa yaliyofanyika katika miji ya Roma na Barcelona walishiriki watu zaidi ya 100,000. Pia yalifanyika maandamano katika miji kadha ya Ujerumani. Kwa mara nyingine Rais Geroge W. Bush alitetea vita vya Iraq wakati akifungua rasmi kampeni yake ya uchaguzi huko Orlando, Florida.