Maambukizi ya Ukimwi huenda yakaongezeka
10 Februari 2025Byanyima amesema huenda ongezeko hilo likatokea ifikapo mwaka 2029 ikiwa Marekani itakatiza mpango mkubwa wa kukabiliana na ugonjwa huo.
Byanyima ameonya kuwa mamilioni ya watu wanaweza kufa na aina mpya sugu ya virusi hivyo inaweza kuibuka.
Katika mahojiano na shirika la habari la AP akiwa nchini Uganda, Byanyima amesema kuwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi yamekuwa yakipungua katika miaka ya hivi karibuni huku visa vipya milioni 1.3 pekee vikirekodiwa mwaka 2023, hili likiwa ni punguzo la 60% tangu maambukizi hayo yalipokithiri mnamo mwaka 1995.
Lakini tangu tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump kwamba nchi yake itakatiza misaada yote ya kigeni ndani ya siku 90, Byanyima amesema maafisa wanakadiria kuwa ifikapo mwaka 2029, huenda kukawa na maambukizi mapya milioni 8.7 ya virusi vya Ukimwi, vifo milioni 6.3 vinavyohusishwa na ugonjwa huo pamoja na mayatima milioni 3.4.