Maafisa wawili wa polisi Tanzania wahukumiwa kifo
23 Juni 2025Mfanyabiashara huyo aliuwawa mwanzoni mwa mwaka 2022, mkoani Mtwara, baada ya kunyang'anywa fedha na mali na maafisa hao.
Kesi hiyo namba 15/2023, imetolewa Hukumu Juni 23, 2025 na Jaji wa Mahakama kuu, kanda ya Dar es salaam Hamidu Mwanga baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri akieleza kuwa watuhumiwa hao wamekiuka kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha makosa ya jinai, namba 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Amesema waliohukumiwa kunyongwa ni Mrakibu wa Polisi Gilbert Kalanje ambaye alikuwa ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mtwara na Mrakibu Msaidizi wa Polisi Charles Onyango aliyekuwa mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara baada ya kubainika kumuua mfanyabiashara huyo Mussa Hamisi kwa kumchoma sindano yenye sumu na kisha kumziba kwa kitambaa puani na mdomoni na kumfungia kwenye chumba mfano wa stoo kwenye kituo cha polisi kilichopo mkoani Mtwara.
Ilipofika majira ya usiku, maafisa hao waliupandisha mwili wa mfanyabiashara huyo kwenye gari la polisi na kwenda kuutupa kusikojulikana.
Wengine waachiliwa huru
Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imewaachia huru maafisa wengine watano wa polisi baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha ushiriki wao kwenye mauaji hayo. Wengine walioachiliwa ni mganga wa hospitali ya polisi na maafisa wa intelejensia wa Jeshi hilo.
Mfanyabiashara wa madini Mussa Hamisi (25) mkazi wa kijiji cha Ruponda wilayani Nachigwea mkoani Lindi aliuawa Januari 5, 2022 na mwili wake kutupwa katika msitu wa Hiari uliopo Kitongoji cha Majengo Kijiji cha Hiari, wilayani Mtwara baada ya marehemu huyo kudai fedha zake zaidi ya shilingi milioni 33.7 zilichukuliwa na maofisa hao wakati walipomfanyia upekuzi.