Maafisa wa Urusi na Marekani wakutana Riyadh kuhusu Ukraine
18 Februari 2025Maafisa wakuu kutoka Urusi na Marekani wamekutana nchini Saudi Arabia leo kuanza mazungumzo juu ya kuboresha uhusiano na kufanya mazungumzo ya kusitisha vita nchini Ukraine. Wajumbe hao wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrovwalikutana katika Ikulu ya Diriyah mjini Riyadh. Rubio aliandamana na mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Mike Waltz na Mjumbe Maalum Steve Witkoff. Lavrov alikuwa na mshauri wa mambo ya nje wa Kremlin, Yuri Ushakov.
Kirill Dmitriev, ni mkuu wa Mfuko wa Uwekezaji wa Urusi ambaye anashiriki mkutano huo. "Maafisa wa Ukraine hawashiriki katika mkutano huo. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema nchi yake haitakubali matokeo ya mazungumzo hayo ya Riyadh ikiwa Kyiv haitashiriki. Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Faisal bin Farhan na mshauri wa usalama wa taifa Musaed al Alban pia walishiriki."
Mkutano huo unaashiria hatua nyingine muhimu ya utawala wa Trump ya kubadili sera ya Marekani ya kuitenga Urusi na inakusudiwa kufungua njia ya mkutano kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Trump mapema mwezi huu aliibadili sera ya Marekani kuhusu Ukraine na Urusi kwa kusema kuwa yeye na Putin wamekubaliana kuanza mazungumzo ya kumaliza vita.