Maafisa wa US na Ukraine wafanya mazungumzo ya amani Saudia
11 Machi 2025Mazungumzo hayo kati ya maafisa wa Ukraine na Marekani yamefanyika katika mji wa bandari katika Bahari Nyekundu wa Jeddah huko Saudi Arabia na yanalenga kuutafutia suluhu mzozo kati ya Urusi na Ukraine ambao ni mkubwa zaidi barani Ulaya tangu vilipomalizika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Marekani imewakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje Marco Rubio na maafisa wengine, huku Ukraine ikiwakilishwa na rais Volodymyr Zelensky akiambatana na mawaziri wake wa ulinzi na mahusiano ya kigeni Andriy Sybiha pamoja na washauri kadhaa wa serikali.
Soma pia: Rais Zelensky awasili Saudi Arabia kwa mazungumzo ya amani
Walipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu matarajio yao katika mazungumzo hayo, Rubio alionyesha kuwa na matumaini makubwa huku maafisa wa Ukraine wakisema baadaye kwamba mkutano huo ulianza chini ya misingi bora yenye kutia moyo. Hata hivyo mshauri wa rais wa Ukraine Andriy Yermak, amesisitiza juu ya umuhimu wa kuwepo kwa dhamana ya usalama akieleza kuwa muhimu zaidi ni kutafuta namna ya kufikia amani ya haki na ya kudumu nchini Ukraine.
Hayo yanajiri wakati pande zote katika mzozo huo zimeshambuliana vikali usiku wa kuamkia leo. Mbali na mashambulizi ya kila siku ya Urusi, Ukraine ilifanya mashambulizi makubwa ya mamia ya droni na kuilenga miji kadhaa nchini Urusi ikiwa ni pamoja na mji mkuu Moscow ambapo watu watatu wameripotiwa kuuawa na wengine 18 wamejeruhiwa. Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema mashambulizi ya Ukraine yanaweza kutatiza mchakato wa usuluhishi.
" Bado hakuna mazungumzo, kwa hivyo hakuna cha kuvuruga bado. Lakini mwelekeo wa usuluhishi unaoonekana kwa sasa unaweza kuharibiwa kwa kiasi kikubwa."
Wakuu wa majeshi wa nchi za Ulaya wakutana Paris kujadili kuhusu dhamana ya usalama kwa Ukraine
Katika hatua nyingine, wakuu wa majeshi wa nchi zaidi ya 30 za Ulaya wanakutana mjini Paris kujadili namna ya kuendeleza uungwaji mkono kwa Ukraine ili kuisaidia kukabiliana na uvamizi wa Urusi. Mazungumzo hayo yatajikita zaidi juu ya namna ya kuunda jeshi la kimataifa litakalokuwa na uwezo wa kuzuia uvamizi mwingine wa Urusi mara baada ya kufikiwa kwa mpango wa kusitisha mapigano.
Soma pia: Ukraine kuwasilisha mpango wa kusitisha vita kwa Marekani
Mkutano huu wa Paris wa wakuu wa majeshi ndio wenye umuhimu zaidi hadi sasa katika jitihada za Ufaransa na Uingereza za kuyahamasisha mataifa mengine ya Ulaya kuunda kile kinachojulikana kama "muungano wa walio tayari" kuilinda Ukraine kwa kuanzisha kikosi maalum ambacho kitatoa hakikisho la usalama ili kuizuia Urusi isiivamie tena Ukraine.
(Vyanzo: Mashirika)