Maafisa wa Marekani wafafanuwa marufuku ya silaha Ukraine
3 Julai 2025Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Sean Parnell, aliwaambia waandishi wa habari hapo jana kwamba wizara yake inaendelea kumshauri Rais Donald Trump juu ya njia zinazofaa za kuipatia msaada wa kijeshi Ukraine, ambazo zinakwendana na dhamira yake ya kuvikomesha vita hivyo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Tammy Bruce, alisema tangazo la Ikulu ya White House halikumaanisha kusitisha moja kwa moja utumaji wa silaha, bali lilihusu tukio moja mahsusi.
Juzi Jummanne, Ikulu hiyo ilisema imezuwia utumaji wa silaha muhimu kuelekea Ukraine, ambazo zilikuwa zimeahidiwa na utawala wa Joe Biden, bila ya kutoa undani wa aina gani za silaha zinahusika na uzuiaji huo.
Jioni ya jana, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alisema maafisa wa serikali yake na wale wa Marekani wanajadiliana kuhusu uamuzi huo.