Maafisa wa Kongo wavamia na kupekua mali za Kabila
18 Aprili 2025Hayo yametokea wakati mwanasiasa huyo alitangaza hivi karibuni kuwa atarejea nchini humo kupitia upande wa masharikiri mwa taifa hilo unaozongwa na mapigano.
Taarifa ya upekuzi huo imetolewa na familia ya Kabila jana jioni. Inaarifiwa maafisa wa usalama walifika kwenye shamba la Kabila la Kingakati umbali wa karibu kilometa 80 kutoka mji mkuu Kinshasa na kumweleza msimamizi wa shamba hilo kuwa upekuzi huo ni zoezi la kawaida. Pia maafisa hao walivamia na kupekua nyumba ya Kabila mjini Kinshasa.
Kulingana na msemaji wa familia hiyo, maafisa hao walisema kwamba wanatafuta vifaa vya kijeshi "vilivyoibwa au kupotea" lakini hawakupata chochote kwenye upekuzi huo.
Rais Felix Tshisekedi wa Kongo amekuwa akimtuhumu Kabila kuwa anapanga "njama za kuiangusha serikali" na pia anawaunga mkono waasi wa M23 wanaopigana na vikosi vya serikali mashariki mwa Kongo.