Maafisa wa Rwanda wawekewa vikwazo kwa mzozo wa Kongo
17 Machi 2025Rwanda inaishutumu Ubelgiji, mkoloni wake wa zamani, kwa kuiunga mkono serikali ya Kinshasa kabla na wakati wa mzozo unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mvutano wa kidiplomasia baina ya Rwanda na Ubelgiji umeongezeka siku za hivi karibuni, wakati uhusiano umekuwa ukidorora kwa muda mrefu. Ikionekana kuwa chanzo cha vikwazo, hasa ndani ya Umoja wa Ulaya, Ubelgiji inashutumiwa na Rwanda kwa kueneza uongo na ghiliba ili kujenga maoni ya chuki yasiyo na msingi dhidi ya nchi yake.
Kwa hiyo Rwanda inamtaka balozi wa Ubelgiji mjini Kigali kuondoka chini ya masaa 48. Waziri wa mambo ya nje wa Ubeljiji, Maxime Prévot amesema hatua ya Rwanda ni uamuzi "usio na uwiano". Na kwa upande wake, Brussels inachukuwa hatua kama hiyo kwa kuwataka wanadiplomasia wote wa Rwanda kuondoka nchini Ubelgiji.
Mwezi Februari, Rwanda tayari ilikuwa imesitisha ushirikiano wa kimaendeleo na Ubelgiji, ikilaani kile ilichokitaja kuwa ni kampeni ya uchokozi ya Brussels dhidi ya Rwanda.
Umoja wa Ulaya, chini ya shinikizo la Ubelgiji haswa, ulipitisha leo Jumatatu vikwazo dhidi ya maafisa wa jeshi la Rwanda kutokana na uungaji mkono wa Kigali kwa waasi wa M23 huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Vikwazo hivyo vinawahusu watu tisa na kampuni moja ya kitaifa nchini Rwanda.
"Lazima sasa usitishaji wa mapigano utekelezwe mara moja"
Baada ya kutolewa vikwazo hivyo, Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot amesema lazima kuweko na mazungumzo baina ya pande hasimu.
"Lazima sasa usitishaji wa mapigano utekelezwe mara moja ili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, makundi ya waasi na Rwanda waweze kufungua njia ya mazungumzo kuelekea amani ya haki na ya kudumu katika eneo hilo."
Miongoni mwa waliowekewa vikwazo ni pamoja na maafisa watatu wa ngazi ya juu wa jeshi la Rwanda, Ruki Karusisi, Eugène Nkubito na Pascal Muhizi, na mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Migodi, Mafuta na Gesi ya Rwanda (RMB), Francis Kamanzi.
Watu wengine waliowekewa vikwazo ni viongozi wa kundi la waasi la M23, akiwemo mkuu wake, Bertrand Bisimwa.
Mazungumzo ya ana kwa ana
Haya yote yanajiri mkesha wa kuanza kwa mazungumzo ya ana kwa ana baina ya serikali ya Kongo na waasi wa M23 chini ya upatanishi wa Angola. Tina Salama, msemaji wa Rais Felix Tshisekedi amesema ujumbe wa Kongo utakuwepo, lakini hakufafanua kuhusu ajenda na majina ya wajumbe wa Kinshasa.
Kwa upande wao waasi wa M23 wamesema watawakilisha ujumbe wa watu watano. Hata hivyo, duru zinasema Corneille Nangaa na Betrand Bisimwa, viongozi wa kundi hilo, hawatoshiriki.
Kuhusiana tu na mzozo huo wa Kongo, mawaziri wa mambo ya nje na wa ulinzi wa jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika SADC na wale wa jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki EAC, wamekutana mjini Harare, Zimbabwe. Mkutano huo unachunguza mapendekezo yaliyotolewa na viongozi wa kijeshi kutoka miungano hiyo miwili kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kutatua mzozo huo.
Licha ya juhudi hizo za kidiplomasia taarifa zinasema kuwa waasi wa M23 wanasonga mbele kwenye uwanja wa mapambano na kukaribia mji wa Walikale, zaidi ya kilomita 100 kaskazini mwa mji wa Goma.