Maafa Afghanistan: Vifo vya tetemeko vyapindukia 1,400
2 Septemba 2025Idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko kubwa la ardhi lililotikisa Afghanistan imeongezeka hadi 1,411, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu la Afghanistan (Afghan Red Crescent Society). Shirika hilo la kibinadamu limesema pia zaidi ya watu 3,124 wamejeruhiwa na zaidi ya nyumba 8,000 zimeporomoka kutokana na tetemeko hilo.
Katika mkoa wa Kunar, ambako ndiko kitovu cha tetemeko hilo lenye ukubwa wa kiwango cha 6, waokoaji wanafanya juhudi za kufika vijiji vya milimani ambavyo bado havijafikiwa. Kwa mujibu wa Ehsanullah Ehsan, mkuu wa idara ya usimamizi wa majanga mkoani humo, operesheni za uokoaji zimekamilika katika vijiji vinne na sasa zinalenga maeneo yaliyo mbali zaidi.
"Hatuna uhakika ni miili mingapi bado imekwama chini ya kifusi,” alisema Ehsan. "Lengo letu ni kukamilisha shughuli hizi haraka iwezekanavyo na kuanza kugawa msaada kwa familia zilizoathirika.”
Changamoto kubwa inayokwamisha juhudi za uokoaji ni barabara nyembamba za milimani na hali mbaya ya hewa, ambazo zimezuia magari kufika maeneo yaliyoathirika. Mashine maalum zimesafirishwa ili kuondoa kifusi barabarani na kurahisisha upatikanaji wa huduma za msaada.
Helikopta za uokoaji na usafirishaji zilionekana zikipeleka misaada na kuwahamisha majeruhi kuelekea hospitali, huku foleni ya magari ya wagonjwa ikijipenyeza kwenye barabara zilizoharibiwa.
Watoto na familia hatarini
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeonya kwamba maelfu ya watoto wako katika hatari kubwa kufuatia maafa haya. Shirika hilo limeanza kusambaza dawa, nguo za kujikinga na baridi, hema, vifaa vya usafi na mahitaji mengine ya dharura.
"Kipaumbele chetu ni kushughulikia mahitaji ya haraka katika afya, maji salama, usafi, lishe, ulinzi wa watoto, makazi ya muda na msaada wa kisaikolojia ili kuhakikisha watoto na familia zao wanapata msaada unaookoa maisha haraka iwezekanavyo,” alisema mwakilishi wa UNICEF nchini humo, Tajudeen Oyewale.
Wanajeshi wa Taliban nao wamesambazwa kusaidia juhudi za uokoaji na kuhakikisha usalama katika maeneo yaliyoathirika. Hata hivyo, hali ya afya nchini humo, ambayo tayari ilikuwa dhaifu kabla ya maafa haya, imezidisha utegemezi wa misaada ya nje, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Changamoto za ufadhili na misaada ya kimataifa
Majanga ya hivi karibuni yamekuja wakati Afghanistan ikiwa bado inapambana na upungufu mkubwa wa misaada ya kibinadamu kufuatia uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, kukata ufadhili wa shirika la misaada la USAID tangu Januari, na kupunguzwa kwa misaada mingine ya kimataifa kutokana na sera za Taliban dhidi ya wanawake na mashirika ya misaada.
Pamoja na changamoto hizo, misaada ya haraka kutoka mataifa mbalimbali imeanza kuwasili. Uingereza imetenga pauni milioni 1 kwa msaada wa dharura kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa na Msalaba Mwekundu wa Kimataifa. India imetuma mahema 1,000 na tani 15 za chakula kuelekea mkoa wa Kunar, huku China ikiahidi kutoa msaada kulingana na mahitaji ya Afghanistan.
Afghanistan, ambayo iko katika eneo linalokumbwa mara kwa mara na mitikisiko ya ardhi, imekuwa ikishuhudia majanga kama haya mara kwa mara. Tetemeko jingine la kiwango cha 6.1 mnamo 2022 liliua watu 1,000 mashariki mwa nchi, likiwa janga la kwanza kubwa kukabili serikali ya Taliban tangu kuchukua madaraka.