M23 yapongeza matarajio ya kuzungumza ya Angola
17 Machi 2025Katika taarifa yake, M23 imesema imepokea vyema tangazo la kufanyika mazungumzo kati yake na serikali ya Kongo yanayotarajiwa katika mji mkuu wa Angola, Luanda lakini ikaibua wasiwasi na kumtaka Rais wa Kongo Felix Tshisekedi kueleza hadharani na kwa uwazi dhamira yake ya kushiriki mazungumzo ya moja kwa moja ambayo M23 imeyataja kuwa muhimu.
Mara kadhaa serikali ya Kongo imekuwa ikikataa kukaa meza moja na waasi wa M23 ambao sasa inawachukulia kama magaidi, lakini Rais wa Angola Joao Lourenco alithibitisha kuwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili yatafanyika, baada ya kumpokea Tshisekedi kwa majadiliano mjini Luanda.
Siku ya Jumanne, Angola ilisema itakuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo katika jitihada za kusitisha mapigano, na baadaye jana ilitoa tarehe ya Machi 18 kama siku yatakayofanyika mazungumzo hayo. Jana vyanzo kutoka Kinshasa vilieleza kuwa serikali ya Kongo inafikiria kutuma wawakilishi kwenye mazungumzo hayo ya amani.
Soma pia: Mazungumzo kati ya serikali ya DRC na M23 kufanyika Luanda
Baadhi ya raia wa Kongo wanapinga hatua ya serikali kuzungumza na M23 kama anavyoeleza mmoja wao kutoka Kinshasa, Jemanuelle Zobela:
"Watu hawa waliwaua kaka zetu, wakawabaka dada zetu na kufanya kila wawezalo kutufanya tusalim amri. Sasa Angola inataka tujadiliane na M23. Na tukikubali kujadiliana na M23, tutabaki kuwa watumwa wa Rwanda na M23, haiwezekani kamwe! Wanataka kutudhibiti. Hapa Kinshasa, tunasema HAPANA kwa wazo la mazungumzo na M23. Wakitaka kujadiliana, waanze kwa kujadiliana na vifo walivyosababisha."
Kikosi cha SADC kujiondoka DRC huku mapigano yakiendelea eneo la mashariki mwa nchi hiyo
Haya yanajiri wakati siku ya Alhamisi, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC ilichukua uamuzi wa kukiondoa kikosi chake cha kulinda amani cha SAMI-DRC huko mashariki mwa Kongo ikitaja kuwa ni katika dhamira ya kufanikisha utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa wakati wa mkutano wa pamoja wa SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC uliofanyika nchini Tanzania.
Hata hivyo, kikosi hicho cha SADC kiliwapoteza makumi ya wanajeshi wake katika vita hivyo hasa ikizingatiwa kuwa katika miezi ya hivi karibuni, M23 imekuwa ikipata mafanikio makubwa katika uvamizi wake kwa kuchukua udhibiti wa miji miwili muhimu ya Goma na Bukavu, hatua ambayo imezusha hofu ya kutokea kwa vita vipana zaidi vya kikanda.
Soma pia: Jumuiya ya SADC yaamua kuondoa vikosi vyake mashariki mwa DRC
Hayo yakiarifiwa, mapigano yanaendelea kuripotiwa mashariki mwa Kongo, vyanzo vya kijeshi vimeeleza kuwa takriban askari 20 wa Burundi wameuawa kufuatia shambulio la M23 huko Kaziba, karibu kilomita 80 kutoka Uvira, mji ulio karibu na mpaka wa Burundi.
Katika hatua nyingine, majenerali watano wa jeshi na polisi la Kongo watafikishwa katika Mahakama Kuu ya Kijeshi mjini Kinshasa leo ili kusomewa mashtaka yanayowakabili baada ya kushindwa kukabiliana na mashambulizi ya waasi wa M23 katika mji wa Goma. Maafisa hao wa ngazi za juu jeshini na kwenye jeshi la polisi wanatuhumiwa kwa woga, ukiukaji wa maagizo, kupoteza vifaa na kukimbia uwanja wa mapigano.
(Vyanzo: Mashirika)