M23 yakubali kuondoka kwa kikosi cha SADC mashariki mwa DRC
29 Machi 2025Waasi wa M23 wamekubaliana na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC, juu ya kuondoka kwa vikosi vyake kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako wanajeshi wake kadhaa waliuawa katika mapigano.
Wakuu wa majeshi wa Afrika Kusini, Zambia, Malawi na Tanzania walikutana na mkuu wa jeshi la M23 Sultani Makenga katika mji wa Goma, kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo.
Pande zote mbili zimekubaliana, kwamba M23 itawezesha kuondoka mara moja kwa askari wa kikosi hicho kupitia uwanja wa ndege wa Goma, ambao kwa sasa hautumiki kwa sababu ya kuharibiwa wakati wa mapigano.
Ujumbe wa SADC nchini Kongo SAMIDRC, unaojumuisha wanajeshi kutoka Malawi, Tanzania na Afrika Kusini, ulitumwa katika eneo hilo Desemba 2023 kusaidia kurejesha amani na usalama.