M23 wasema wanakusudia kwenda hadi Kinshasa
30 Januari 2025Kwa mujibu wa dondoo za mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na uongozi wa waasi wa M23 mjini Goma mchana wa Alkhamis (Januari 30), kundi hilo lilisema kuutwaa kwao mji huo muhimu halikuwa jambo la bahati mbaya na kwamba wangeliendelea kubakia hapo muda wote.
Vile vile, waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda walisema kwamba lengo lao la sasa sio tu kuushikilia mji wa Goma pekee, bali pia kusonga mbele hadi makao makuu ya nchi, Kinshasa.
Soma zaidi: Uingereza yatishia kuikatia misaada Rwanda kwa yanayojiri Goma
Akizungumza na waandishi hao wa habari, mkuu wa muungano ya makundi yenye silaha unaolihusisha pia kundi la M23, Corneille Nangaa, alisema: "Tutaendelea na maandamano ya ukombozi moja kwa moja hadi Kinshasa."
Wachambuzi wanasema kauli hii inaweza kumaanisha kuwa waasi hao wana dhamira ya kuiondosha madarakani serikali, jambo ambalo linautanuwa zaidi mzozo huo.
Ufaransa yataka wanajeshi wa Rwanda waondoke Kongo
Hayo yakijiri, Ufaransa, ambayo inaendesha kampeni ya kidiplomasia kusaka suluhisho la mzozo huo, ilivitaka vikosi vyote vya Rwanda na vya wapiganaji wa M23 viondoke mashariki mwa Kongo ili kuhakikisha upatikanaji wa amani.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa, Christophe Lemoine, alisema hayo baada ya waziri wake, Jean-Noel Barrot, kuondoka kwa ziara ya eneo la Maziwa Makuu kuushughulikia mzozo huo.
Soma zaidi: Kiongozi wa DRC asema jeshi lake linapambana vikali dhidi ya mashambulizi ya M23
"Heshima na mamlaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo si suala la kujadiliana." Alkisema Lemoine.
Ziara ya Barrot inafanyika baada ya Rais Emmanuel Macron kuzungumza kwa njia ya simu na Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Felix Tshisekedi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya serikali ya Kongo, Barrot aliwasili mjini Kinshasa siku ya Alkhamis (Januari 30), ambako atafanya mazungumzo na Rais Felix Tshisekedi.
Ziara ya Barrot, ambaye nchi yake imelaani vikali kusonga mbele kwa waasi wa M23 kuingia mji wa Goma, inakusudiwa kuunga mkono juhudi kama hizo zilizochukuliwa na Angola na Kenya.
Tshisekedi aikosowa jumuiya ya kimataifa
Haya yanajiri ikiwa ni siku moja tu tangu Rais Tshisekedi kuhutubia taifa na kuelezea kile alichosema ni utayarifu wa jeshi lake kukabiliana na waasi wa M23 na kuyarejesha maeneo yote wanayoyakalia.
Kwenye hotuba hiyo ya kwanza tangu M23 waitwae Goma, Tshisekedi aliikosowa vikali jumuiya ya kimataifa kukaa kimya na kutochukuwa hatua, akisema jumuiya hiyo inaangalia tu kwa macho wakati hali ikizidi kuwa mbaya mashariki mwa Kongo.
Soma zaidi: Duru: Waasi wa M23 waanza kuelekea Bukavu
Tshisekedi alikataa kushiriki mkutano wa dharura wa jana uliokuwa umeitishwa na mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais William Ruto wa Kenya, kuijadili hali ya mashariki mwa Kongo.
Vyanzo vya habari kwenye eneo hilo vilivyonukuliwa na shirika la habari la AFP vinasema waasi wa M23 wanasonga mbele sasa kuelekea tayari wamezitwaa wilaya nyengine mbili kwenye jimbo la Kivu Kusini.
Jeshi la Kongo, ambalo maafisa wake kadhaa wanaripotiwa kujisalimisha kwa waasi wa M23, bado halijatowa tamko lolote hadi sasa juu ya kusonga mbele kwa waasi hao.
Baada ya siku kadhaa za makabiliano ya hapa na pale yaliyopoteza maisha ya watu zaidi ya 100 na wengine wanaokaribia 1,000 kujeruhiwa, baadhi ya wakaazi wa mji huo wa Goma wamejitokeza mitaani kusaka huduma na bidhaa za kuweka akiba, wakiwa na wasiwasi wa yatakayokuja baadaye.