M23 waanzisha mapigano mapya Kongo
6 Februari 2025Vyanzo vinane vya habari vimeeleza jana kuwa waasi wa M23 wameuteka mji wenye utajiri wa madini katika jimbo la Kivu Kusini, wakianzisha tena harakati za kuelekea mji mkuu wa jimbo hilo, Bukavu, na hivyo kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano walioyatangaza wenyewe wiki hii.
Duru za kiusalama na kiutu zimeliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa mapigano makali yalizuka alfajiri ya Jumatano, wakati wapiganaji wa M23 na vikosi vya Rwanda walipouteka mji wa Nyabibwe, uliopo umbali wa kilomita 100 kutoka Bukavu na kilomita 70 kutoka uwanja wa ndege wa jimbo hilo.
DRC: Usitishaji mapigano ilikuwa njama ya M23
Kundi la M23 lilipotangaza kusitisha mapigano, lilisema halina nia ya kuchukua udhibiti wa Bukavu au maeneo mengine.
Hata hivyo, Msemaji wa Serikali ya Kongo, Patrick Muyaya, amesema usitishaji huo wa upande mmoja ulikuwa ni njama. Katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu ya mapigano kati ya M23 na jeshi la Kongo, makubaliano kadhaa ya usitishaji mapigano yalitangazwa lakini yalivunjika mara kwa mara bila kutekelezwa.
Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye anakanusha nchi yake kuiunga mkono M23, ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano katika ukanda huo na kufikiwa suluhisho la amani ya kudumu. Kagame na Rais mwenzake wa Kongo, Felix Tshisekedi wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuia ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC jijini Dar es Salaam, Tanzania siku ya Jumamosi. Ijumaa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa litakutana kwa kikao maalum kuujadili mzozo huo, kwa ombi la Kongo.
Watu 2,900 wameuawa
Hayo yanajiri wakati ambapo Umoja wa Mataifa umesema kuwa mapigano katika mji wa Goma yamesababisha mauaji ya takribani watu 2,900. Naibu Mkuu wa Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Kongo, MONUSCO, Vivian van de Perre alisema Jumatano kuwa miili 2,000 tayari imeshapatikana katika mitaa ya Goma, na miili mingine 900 bado imebaki kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti katika hospitali za Goma, na kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka.
''Bado kuna miili mingi iliyoharibika katika maeneo kadhaa. Kwa hivyo Shirika la Afya Duniani lina wasiwasi kuhusu aina ya miripuko ya magonjwa inayoweza kutokea,'' alifafanua van de Perre.
Wakati huo huo, waendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC wamesema katika taarifa yao kwamba wanafuatilia kwa ukaribu matukio yanayoendelea mashariki mwa Kongo, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ghasia katika wiki zilizopita, hasa katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma.
Kulingana na ICC, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama hiyo, Karim Khan anayechunguza uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu, tayari ameanzisha uchunguzi kuhusu madai ya uhalifu ulioanza kufanywa tangu mwanzoni mwa mwaka 2022.
Uchunguzi wa ICC unaendelea
ICC imesema uchunguzi huo unaendelea, kwa udharura na kuzingatiwa, huku waendesha mashtaka wakitoa wito wa kupewa taarifa na ushahidi.
Katika hatua nyingine, Malawi imeamuru wanajeshi wake kuanza kuondoka mashariki mwa Kongo, ambako M23 wameanzisha mapigano mapya. Ofisi ya Rais Lazarus Chakwera, Jumatano usiku ilimuamuru kamanda wa Jeshi la Ulinzi la Malawi kuanza mchakato wa kuwaondoa wanajeshi hao, ili kuheshimu tamko la kusitisha mapigano.
AFP, AP, Reuters