M23 kujiondoa kwenye mji wa Walikale kwa ajili ya amani
23 Machi 2025Muungano wa makundi ya waasi wa AFC/M23 umesema katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye jukwaa la X, kwamba umeamua kuviondoa vikosi vyake kutoka kwenye mji wa Walikale na pia kutoka kwenye maeneo ya jirani ya mji huo.
Uamuzi huu unaambatana na hatua ya kusitisha mapigano iliyotangazwa mwezi Februari na ni hatua ya kuunga mkono mipango ya kuleta amani. Kauli ambayo imepokelewa kwa mashaka na maafisa wa jeshi la Kongo.
Mwanachama mmoja mkuu wa muungano wa AFC/M23 ambaye hakutaka kutajwa jina amesema kuvihamisha vikosi vyake kunamaanisha "kuipa amani nafasi".
Mpaka sasa haijulika ni wapi waasi wa M23 watavipeleka vikosi vyake baada ya kuviondoa kutoka kwenye mji wa Walikale.
Serikali kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema inatumai kwamba M23 itakamilisha hatua hiyo kiuhalisia baada ya kundi hilo mnamo wiki hii kujiondoa katika dakika za mwisho kwenye mazungumzo na serikali ya Kongo huko nchini Angola kutokana na vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya baadhi ya viongozi wake pamoja na maafisa wa Rwanda.
Soma pia: UN: Vita vya mashariki mwa DRC vimesababisha watu 100,000 kukimbilia nchi jirani
Mazungumzo hayo yangekuwa ni ya kwanza ya moja kwa moja na serikali ya Kongo baada ya Rais Felix Tshisekedi kubadili msimamo wake wake wa muda mrefu wa kukataa kuzungumza na waasi wa M23.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo Therese Kayikwamba Wagner, amewaambia waandishi wa Habari kwamba serikali inasubiri kwa hamu kuona kama kweli M23 watajiondoa kutoka kwenye mji wa Walikale na pia iwapo kundi hilo litayapa kipaumbele mazungumzo pamoja na amani ya Kongo.
Hata hivyo kiongozi wa muungano wa M23 Corneille Nangaa, mnamosiku ya Ijumaa alipuuzilia mbali wito wa pamoja wa kusitisha mapigano mara moja kati ya Kongo na Rwanda na badala yake alisisitiza umuhimu wa mazungumzo ya moja kwa moja na serikali kuu ya mjini Kinshasa, akisema hiyo ndio njia pekee ya kuutatua mzozo.
Juhudi za kuleta Amani
Kumekuwa na majaribio kadhaa ya kutatua migogoro iliyotokana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 kati ya Rwanda na Kongo pia migogoro inayohusiana na ushindani wa utajiri wa madini- miongoni mwa juhudi za amani ni pamoja na kufikiwa makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano ambayo yalikiukwa na pia mikutano ya kilele ya kikanda iliyoandaliwa kwa ajili ya kufungua mazungumzo.
Soma pia: M23 yaingia katika mji mwingine Mashariki mwa Kongo wa Walikale
Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Umoja wa Mataifa na serikali za nchi za Magharibi zinasema Rwanda imekuwa ikitoa silaha na wanajeshi wake kwa kundi la M23 linaloongozwa na Watutsi. Kwa upande wake Rwanda inakanusha hili, ikisema, jeshi lake limekuwa linachukua hatua za kujilinda dhidi ya jeshi la Kongo na makundi ya wanamgambo yaliyoanzishwa na wahusika wa mauaji ya kimbari.
Vyanzo: RTRE/AFP