Lula asema ikiwa Trump atapandisha ushuru, Brazil itajibu
31 Januari 2025Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amesema kuwa ikiwa Rais wa Marekani Donald Trump atapandisha ushuru kwa bidhaa za Brazil, atajibu kwa kulipiza kisasi, lakini alisisitiza kuwa angependa kuboresha uhusiano badala ya kuanzisha vita vya biashara.
Lula alisema angetaka kuboresha uhusiano wa kibiashara na Marekani, ambayo ni mshirika wa pili kwa ukubwa kibiashara wa Brazil baada ya China. Amesema anataka kuiheshimu Marekani na Trump aiheshimu Brazil.
Soma pia: Lula awarai viongozi wa G20 kutokomeza njaa na umasikini
Lula alikosoa uamuzi wa Trump wa kujitoa kwenye makubaliano ya Tabianchi ya Paris, na kuutaja kuwa hatua ya kurudi nyuma kwa ustaarabu wa binadamu, huku pia akiyakosoa mataifa tajiri kwa kushindwa kutimiza ahadi zao za kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.