Lukashenko arefusha utawala wake madarakani Belarus
27 Januari 2025Lukashenko ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka wa 1994, ameshinda uchaguzi ulioshutumiwa na Umoja wa Ulaya na wapinzani walioko uhamishoni au magerezani. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni ya waliopiga kura Jumapili, mtawala huyo mwenye umri wa miaka 70 alionekana kushinda kwa asilimia 87.6 ya kura.
Lukashenko aliendesha operesheni kali ya ukandamizaji dhidi ya wapinzani tangu maandamano makubwa yaliyofanywa dhidi yake mwaka wa 2020. Mara hii, wagombea waliochaguliwa kusimama dhidi yake walifanya kampeni za kumuunga mkono. Kiongozi wa upinzani aliyeko uhamishoni Svetlana Tikhanovskaya ameuita uchaguzi huo kuwa kituko, wakati Umoja wa Ulaya ukiutaja udanganyifu. Lukashenko, hata hivyo amesema hajali ikiwa umoja huo unayatambua matokeo hayo au la.
Katika uchaguzi wa mwaka 2020 wapinzani wake na mataifa ya magharibi walidai kuwa Lukashenko alifanya udanganyifu ambapo mamlaka zilianza kufanya msako wa waandamanaji na wapinzani wa kiongozi huyo.