Lugha ni kijerumani tu wakati wa shule nchini Ujerumani
27 Januari 2006Wengi wa wanafunzi katika shule hiyo wanatoka kwenye familia za wakimbizi na hatua hii ya kuwataka wanafunzi wote katika shule hiyo kutumia lugha ya kijerumani tu bila ya kutumia lugha nyingine hata wakati wa mapumziko shuleni hapo, imesababisha kuwepo kwa kauli mbalimbali za kisiasa.
Kaimu mkuu wa shule hiyo, Hans-Joachim Schriefer anasema amri hiyo ya kuwataka wanafunzi watumie lugha ya kijerumani tu, imeridhiwa na wawakilishi wa wazazi pamoja na wanafunzi.
Kaimu mkuu huyo wa shule ya sekondari ya Herbert Hoover, anasema wamefanya uamuzi huo kwa sababu kwa kawaida shuleni hapo kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi ambao si wajerumani na wanafunzi hao wa kigeni wamekuwa wakizungumza karibu lugha 12 tofauti ikiwemo inayotumika sana ya kituruki.
Schriefer anasema lengo la kuwataka wanafunzi watumie kijerumani katika shule hiyo ni kuwarahisishia lugha ya mawasiliano kwa kuwa wote wataelewana kwa kutumia lugha moja na kuwasaidia wapate alama nzuri katika masomo kwani lugha ya kufundishia shuleni hapo ni kijerumani.
Hatua hiyo imeungwa mkono na serikali inayoongozwa na Bi.Angela Merkel lakini haijaifurahisha jumuiya ya waturuki waishio Berlin.
Mbunge wa Uturuki kutoka chama cha upinzani cha ulinzi wa mazingira, Ozcan Mutlu amesema amri hiyo inapingana na katiba ya Ujerumani ambayo inasema kwamba mtu yeyote hatakiwi kubaguliwa kwa sababu ya lugha anayoitumia.
Wanafunzi wenyewe wana mtazamo tofauti juu ya amri hiyo mpya. Mwanafunzi wa ki-Pakistani mwenye umri wa miaka 17 aitwaye Assad anasema kama wanataka kupata nafasi ya mafunzo ya kazi ni lazima wajue kuzungumza kijerumani.
Lydia ni mwanafunzi mwingine, ana asili ya Uturuki na umri wa miaka 13, anasema anaelewa umuhimu wa kutakiwa kuzungumza kijerumani darasani lakini si wakati wa mapumziko.
Kaimu mkuu wa shule hiyo anaeleza kwamba, wakimuona mwanafunzi haongei kijerumani shuleni hapo, hawamuadhibu ila wanamuita na kumuomba atumie lugha ya kijerumani.
Sheria hii pekee ya kijerumani ilianzishwa mwaka mmoja uliopita, lakini makala iliyoandikwa hivi karibuni katika gazeti la kituruki la Hurriyet kuhusu shule hiyo ya Herbert Hoover, imezusha tena mjadala uliopita kuhusu matumizi ya lugha kama njia ya kuwalazimisha wakimbizi milioni 4.7 waliopo Ujerumani kuungana.
Katibu wa dola anayeshughulikia masuala ya wageni katika ofisi ya kansela, Maria Boehmer, hajazungumzia tu kuhusu kuiunga mkono hatua iliyochukuliwa na shule ya sekondari ya Herbert Hoover, lakini pia ameonyesha matumaini kwamba shule nyingine zitaifuata hatua hiyo.
Katibu huyo anasema watoto wanatakiwa wapewe fursa zote za kuwafanya wawe wanajamii wa kijerumani waliokamilika na hii inamaanisha ni lazima waijue vema lugha ya kijerumani.
Naye makamu wa spika wa bunge nchini Ujerumani, Wolfgang Thierse ameiunga mkono amri hiyo na kuitaka itekelezwe katika shule zote nchini Ujerumani ili kuonyesha kuwa wajerumani wako makini katika suala la muungano.
Wajerumani wameanza tena kujiuliza ikiwa suala la kuwaunganisha wakimbizi lilifanikiwa mwaka uliopita pale zilipozuka vurugu katika maeneo ya wakimbizi pembezoni mwa jiji la Paris nchini Ufaransa, kumekuwa na hofu kuwa huenda hali kama hiyo iliyotokea Ufaransa itatokea nchini Ujerumani.
Suala la lugha limebaki kuwa kitovu cha majadiliano hayo, na shule nyingine huko Berlin ambayo ni mojawapo ya shule zenye wanafunzi wengi wa kituruki mjini humo, nayo imeanza kuwalazimisha wanafunzi wake wazungumze kijerumani tu wawapo shuleni.
Lakini hata hivyo viongozi katika miji mingine mikubwa nchini Ujerumani yenye idadi kubwa ya wakimbizi ikiwemo Frankfurt, Cologne, Hamburg na Munich, wamesema hawawezi kuwazuia wanafunzi kutumia lugha nyinginezo wakati wa mapumziko kwenye viwanja vya shule.