London:Bush awasili leo Uingereza:
18 Novemba 2003Rais George W. Bush wa Marekani atawasili London leo jioni kuanza ziara yake ya pili nchini Uingereza akiwa ni Rais. Mwezi wa Julai mwaka wa juzi, miezi sita baada ya kuapishwa kwake, yeye pamoja na mke wake walikula chakula cha mchana na Malkia Elizabeth II katika Kasri la Buckingham. Rais Bush atakuwa mjini London hadi siku ya Ijumaa akiwa mgeni mahsusi wa Malkia Elizabeth 11. Atazungumza na Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, kuhusu mustakabali wa Irak baada ya Marekani kutangaza mwishoni mwa juma kuwa itaharakisha kuwapa madaraka Wairak ili waweze kuitawala nchi yao. Masuala mengine watakayozungumzia ni mgogoro kati ya Waisraeli na Wapalestina na vita vya biashara ya vyuma kati ya Marekani na nchi za Ulaya. Wakuu wa polisi mjini London wamesema kuwa Polisi wapatao 14,000 watashika doria wakati wa ziara yake.