London yaandaa mkutano kutafuta njia ya kumaliza vita Sudan
15 Aprili 2025Maafisa waandamizi kutoka nchi mbalimbali wamekusanyika jijini London Jumanne hii, wakilenga kuweka mkakati wa kuleta amani nchini Sudan wakati taifa hilo linaadhimisha miaka miwili tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hata hivyo, pande mbili zinazopigana –jeshi la kawaida la Sudan na wanamgambo wa RSF – hazihudhurii mazungumzo hayo.
Vita hivyo vilianza Aprili 15, 2023 kufuatia mvutano wa madaraka kati ya majenerali wawili waliokuwa washirika wa karibu, ambao sasa wamegeuka kuwa mahasimu wakubwa: Jenerali Abdel Fattah al-Burhan wa jeshi la taifa na Mohamed Hamdan Daglo (Hemedti) wa kikosi cha RSF. Umoja wa Mataifa umeyataja mapigano hayo kama chanzo cha janga kubwa zaidi la njaa na wakimbizi duniani kwa sasa.
Maafa makubwa na hali ya kibinadamu kuzorota
Vita hivi vimesababisha zaidi ya watu milioni 13 kufungasha virago, huku makumi ya maelfu wakiuawa. Marekani imezituhumu pande zote mbili kwa kuhusika na ukatili dhidi ya raia. Shirika la UNICEF limesema kuwa maisha ya mamilioni ya watoto Sudan yameporomoka, likikadiria kuwa watoto wapatao 2,776 waliuawa au kujeruhiwa kati ya 2023 na 2024 — ongezeko kubwa kutoka visa 150 vilivyothibitishwa mwaka 2022.
Tathmini iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa baa la njaa limekwisha athiri baadhi ya maeneo nchini humo. Zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada wa dharura, huku wanawake na wasichana milioni 12 wakikabiliwa na hatari ya ukatili wa kijinsia.
Soma pia: Baada ya miaka miwili ya vita, Sudan bado haina dalili ya kufikia amani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy, ametangaza msaada mpya wa pauni milioni 120 (sawa na dola milioni 158) kwa ajili ya kusaidia juhudi za kibinadamu nchini Sudan. "Uingereza haitaruhusu Sudan isahaulike,” alisema Lammy, akisisitiza kuwa amani ya Sudan ni muhimu kwa usalama wa kimataifa.
Majukumu ya kimataifa, mvutano wa uwakilishi
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, huku mataifa mengine kama Marekani na Saudi Arabia yakishiriki. Viongozi wa mashirika ya kimataifa, yakiwemo Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), nao wanahudhuria.
Hata hivyo, serikali ya Sudan imepinga kutoshirikishwa kwake katika mkutano huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ali Youssef, alimtumia barua Lammy akilalamika kuwa mkutano unafanyika bila idhini au uwepo wa serikali ya Sudan, akidai kuwa hatua hiyo inaipa RSF hadhi sawa na ya dola ya Sudan. Lakini Ujerumani imesema pande zote – jeshi na RSF – hazikuwa tayari kushiriki mazungumzo hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, ameutaja mzozo wa Sudan kuwa "janga kubwa zaidi la kibinadamu katika wakati huu,” na kuahidi msaada wa euro milioni 125 (dola milioni 142). Kwa upande wake, Rais wa ICRC, Mirjana Spoljaric, amesema miaka miwili ya vita imewaacha raia wa Sudan "wakiwa wamekwama katika ndoto mbaya isiyoisha ya kifo na uharibifu.”
Soma pia: Sudan yaiambia korti ya ICJ kwamba UAE ndio "nguvu inayoendesha" mauaji ya halaiki
Mapigano haya yametokana na kuzorota kwa uhusiano kati ya Burhan na Daglo kufuatia mapinduzi ya mwaka 2021, yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa mpito aliyekuwa amewekwa baada ya kupinduliwa kwa dikteta wa muda mrefu Omar al-Bashir mwaka 2019. Kwa sasa, jeshi linadhibiti maeneo ya mashariki na kaskazini, huku RSF wakidhibiti maeneo makubwa ya Darfur na baadhi ya sehemu za kusini, hali inayoifanya Sudan kugawanyika kiutawala.
Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia siasa, Bankole Adeoye, amesema amani ya kweli Sudan inahitaji kila sauti kusikika na kila upande kushiriki katika kuijenga upya nchi hiyo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, naye ameonya kuhusu uingizwaji wa silaha na wapiganaji nchini humo, akitaka msaada wa nje na uhamishaji wa silaha usitishwe mara moja.